Banka Aibuka Yanga Awaomba Radhi Mashabiki wa Jangwani - Karafuu24 Blog

Breaking

Friday, 2 November 2018

Banka Aibuka Yanga Awaomba Radhi Mashabiki wa Jangwani

Banka Aibuka Yanga Awaomba Radhi Mashabiki wa Jangwani
KIUNGO wa Yanga, Mohamed Issa ‘Mo Banka’ ameibuka na kuomba msamaha kwa mashabiki wa timu hiyo huku akiahidi kurejea kwa nguvu zote mara baada ya kumaliza adhabu yake.

Kamati ya Kuzuia na Kupambana na Dawa Zisizoruhusiwa Michezoni ya Kanda ya Tano Afrika (RADO) ilimfungia kwa miezi 14 kiungo huyo wa kimataifa wa Tanzania baada ya kumkuta na hatia ya kutumia mihadarati.

Banka aliyesajiliwa Yanga SC Julai mwaka huu kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro, alikutwa na hatia ya kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni, aina ya Bangi Desemba 9 mwaka jana baada ya kufanyiwa vipimo wakati wa michuano ya Cecafa Chalenge nchini Kenya.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, kwa niaba ya kiungo huyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten alisema kuwa kama uongozi tayari umesamehe Banka baada ya kukiri kufanya kosa hilo huku akiahidi kutorudia tena.

Ten alisema, kiungo ameahidi kurejea uwanjani kwa nguvu zote Februari 8, mwakani mara baada ya adhabu yake kumalizika atakapomaliza kifungo chake cha miezi 14 alichopewa baada ya kukutwa na hatia hiyo.

Aliongeza kuwa, kiungo huyo anaahidi kubadilika huku akiomba ushirikiano wa kutosha kutoka kwa mashabiki wa Yanga akiwa katika kipindi kigumu akiwa mbali na timu.

“Banka hivi sasa haruhisiwi kufanya chochote kitakachohusiana na soka hata kufanya mazoezi ya binafsi zaidi ya kukaa pekee lakini ameahidi kurejea kwa nguvu za kutosha kuipambania timu hiyo mara baada ya kumaliza adhabu yake.

“Banka ni kati ya wachezaji wetu wa Yanga tuliowasajili katika msimu huu kabla ya kukutwa na hatia hiyo na kupewa adhabu, hivyo bado mchezaji halali.

No comments:

Post a Comment