STEVE NYERERE AMMALIZA WEMA - Karafuu24 Blog

Breaking

Wednesday, 31 October 2018

STEVE NYERERE AMMALIZA WEMA

Image result for wema na steve nyerere
SIKU chache baada ya staa wa filamu za Kibongo, Wema Isaac Sepetu kukumbwa na msala wa kufungiwa na Bodi ya Filamu Tanzania, mwigizaji mwenzake ambaye ni rafiki yake aliyefikia hatua ya kuitana ndugu, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ ameibuka na kummaliza kabisa mwanadada huyo.  

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, Steve alisema kuwa, Wema ni rafiki yake, wamefanya kazi pamoja na wamekuwa kama ndugu na ni kila kitu kwake, lakini kwa hili alilofanya kwa sasa la kuachia video chafu akiwa na mpenzi wake hakubaliani nalo kwani limechafua taifa.

Steve alieleza kwamba, Wema ni staa ambaye anazungumziwa Tanzania, Kenya, Uganda na nchi nyingine hivyo anaipeperusha bendera ya taifa. Alisema kwa aibu hiyo aliyoileta kwa jamii, Wema hafai kufumbiwa macho wala kuhurumiwa. “Wema ni mtu mzima na ana akili zake timamu, lakini amefanya ujinga ambao ni aibu kwa sisi wasanii wenzake na taifa, hapa asimsingizie shetani bali ajilaumu mwenyewe maana alijua anachokifanya kuwa ni kosa,” alisema Steve.

ADHABU NI NDOGO
Steve alizidi kutiririka kuwa, adhabu aliyopewa Wema na Bodi ya Filamu ya kufungiwa, ni ndogo na anastahili adhabu kubwa zaidi ili iwe fundisho kwa wengine maana wanaharibu vizazi vijavyo.
“Kwanza niseme tu adhabu zinazotolewa kwa Wema siyo kwamba anaonewa bali ni kwa ajili ya kuwanusuru watoto wetu jamani, naona hii adhabu ya kufungiwa kufanya filamu ni ndogo, alistahili kubwa ya hali ya juu na hapo bado TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) nao watakuja na adhabu yao.
“Ninaomba wahusika watoe adhabu kulingana na kiwango cha makosa yanayofanywa, maana kwa Wema ingekuwa ilitokea bahati mbaya sawa, lakini kwake aliyataka mwenyewe bila kujali kwamba yeye ni mtu mzima ambaye mama yake anamtegemea, ndugu na hata Watanzania wapo wanaotamani kuwa na hadhi kama aliyonayo,” alisema Steve.

Kwa upande mwingine Steve aliwataka wasanii kuheshimu miiko na kuzingatia maadili ya Kitanzania na ustaa wao wasiuelekeze kwenye mambo yasiyofaa bali wawe kioo cha jamii kweli maana wanatazamwa na jamii nzima, yaani watoto na watu wazima.

Wiki iliyopita Wema alifungiwa kujishughulisha na sanaa kutokana na video yake chafu na aliyekuwa akimwita ‘future husband’ wake, Patrick Christopher ‘PCK’ kusambaa kwenye mitandao ya kijamii huku wakati huohuo akiwa anasubiri adhabu nyingine kutoka kwa TCRA ambao tayari wameshamfungulia kesi Polisi.
Stori:GLADNESS MALLYA, RISASI MCHANGANYIKO

No comments:

Post a Comment