ZFA yasema haijapata taarifa za kufungiwa ‘Banka’ - Karafuu24 Blog

Breaking

Thursday, 6 September 2018

ZFA yasema haijapata taarifa za kufungiwa ‘Banka’


NA AMEIR KHALID
CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA), kimesema, hakijapata taarifa rasmi ya kufungiwa kwa kiungo wa timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, Mohamed Issa ‘Banka’.
Akizungumza na gazeti hili,Katibu wa Kamati ya muda ya ZFA, Khamis Abdalla Said, alisema, licha ya taarifa hizo kuenea kwa baadhi ya vyombo vya habari, lakini, ZFA bado haijapokea taarifa yoyote kutoka CAF au Cecafa.
Alisema kuwa wao kama chama hawezi kuzungumzia kwa urefu jambo hilo, hadi pale watakapopata taarifa ya maandishi kutoka CAF au Cecafa.
Hivyo, aliwataka Wazanzibari na wapenda soka kwa ujumla kuwa wastahamilivu hadi pale watakapopokea taarifa hizo.
Juzi, baadhi ya vyombo vya habari yakiwemo magazeti yaliandika kuwa kiungo huyo wa Yanga, amefungiwa kucheza soka na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa muda mwaka mmoja.
Taairfa hizo zilieleza kuwa Banka amefungiwa kwa kosa la kufeli kwa vipimo ambavyo viliendeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika michuano ya CECAFA Chalenji, iliyofanyika mwaka jana nchini Kenya.
Taarifa zilisema kuwa timu ya Zanzibar na klabu ya Mtibwa walipewa majibu kuhusu vipimo hivyo, ndiyo maana klabu ya Mtibwa Sugar haikuweza kumtumia kiungo huyo tangu Februari 2018.
Lakini, hivi karibuni uongozi wa  timu yake ya sasa ya Yanga ulisema kuwa Banka yupo kwao Zanzibar akiiguza majereha ya goti na ikitajwa kuwa sababu ya kuendelea kukosekana kwenye kikosi cha Yanga.
Uongozi huo  kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu Omary Kaya, umenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa, hautazungumzia lolote juu ya suala la kufungiwa kwa mchezaji huyo.
Kaya ameeleza kuwa hawatasema lolote huku wakisubiri kauli husika kutoka kwa shirikisho la soka Tanzania (TFF) kuwapa ukweli kuhusu suala hilo kama amefungiwa au sivyo.

No comments:

Post a Comment