Polisi Yamshikilia Mwanaume Anayewawekea Dawa ya Kulevya Wanawake na Kuwabaka - Karafuu24 Blog

Breaking

Saturday, 15 September 2018

Polisi Yamshikilia Mwanaume Anayewawekea Dawa ya Kulevya Wanawake na Kuwabaka

Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza linawashikilia watu watatu ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya kihalifu katika maeneo mbalimbali mkoani humo, akiwemo mtuhumiwa wa tukio la ubakaji.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa  Mwanza, Jonathan Shanna, amemtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni  Kennedy Obworo, mwenye umri wa miaka 35, ambaye amekuwa akiwawekea wanawake dawa za kulevya katika vinywaji na kisha kuwabaka na kuwaibia vitu walivyonavyo.

Katika tukio jingine, jeshi hilo linamshikilia Sheshe Mazoya, anayedaiwa kuwa  mganga wa kienyeji mkazi wa Wilaya ya Magu kwa kosa la kukutwa na nyara mbalimbali za serikali ikiwemo mikia miwili ya nyumbu na pembe moja ya swala, kucha za Simba na miiba ya nungunungu ambavyo alikuwa anavimiliki kinyume na sheria.

Aidha, Kamanda Shanna amesema wanamshikilia mwanamke anayefahamika kwa jina la Sonia Fanuel kwa kosa la wizi wa kufungua milango kwa kutumia funguo bandia.

Kamanda Shanna ambaye amechukua nafasi ya Kamanda Ahmed Msangi aliyehamishiwa makao makuu, amesema watuhumiwa wote  wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani Jumatatu ijayo kujibu  tuhuma zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment