KIBA AANZA KAZI COASTAL UNION - Karafuu24 Blog

Breaking

Monday, 3 September 2018

KIBA AANZA KAZI COASTAL UNION


Mshambuliaji mpya wa timu ya Coastal Union, Ali Saleh Kiba ‘Alikiba’, ameanza kazi rasmi leo Jumatatu baada ya kumaliza majukumu yake ya kimuziki.

Alikiba licha ya kuwa mchezaji lakini inaelezwa ni mmoja wa wadhamini wa timu hiyo kupitia kinywaji chake cha Mo Faya na hakuweza kujiunga na timu hiyo kwa wakati kutokana na kuwa na ziara ya kimuziki nje ya nchi kabla ya juzi Jumamosi kuwepo uwanjani kuishuhudia timu yake ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kwa mujibu wa Kocha Mkuu, Juma Mgunda alisema kuwa ameshindwa kumtumia mchezaji huyo katika mchezo huo kutokana na kukosa utimamu wa mwili kwa kuwa hajaungana na timu kwa wakati huku akisisitiza timu yake haiwezi kumtegemea mchezaji mmoja.

“Alikiba ni mmoja tu kati ya wachezaji 30 ambao tumesajili kwa ajili ya msimu mpya wa ligi kuu, angalia leo hakucheza lakini siyo peke yake, wapo wachezaji kibao ambao hawajaweza kucheza na ikifika wakati wake wa kucheza atacheza.

“Kikubwa ukiangalia hakuwa na utimamu kwa kuwa hakuwa kwenye timu, hivyo asingeweza kucheza ila yeye ataanza mazoezi rasmi kesho (leo) na huenda nikaanza kumtumia katika mechi zinazofuata kwa sababu ni mchezaji mzuri ambaye ananisaidia,” alisema Mgunda

No comments:

Post a Comment