DK.SHEIN AZUNGUMZA NA UJUMBE WA ASKOFU MKUU WA KANISA LA ANGIKANA TANZANIA, - Karafuu24 Blog

Breaking

Monday, 10 September 2018

DK.SHEIN AZUNGUMZA NA UJUMBE WA ASKOFU MKUU WA KANISA LA ANGIKANA TANZANIA,

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dkt. Maimbo  Willium Mndolwa (kulia) wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na Viongozi mbali mbali wa Kanisa hilo leo,[Picha na Ikulu.]10/09/2018.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akizungumza na Uongozi wa  Kanisa la Anglikana Tanzania ulioongozwa na  Askofu Mkuu wa kanisa hilo  Dkt. Maimbo  Willium Mndolwa (wa nne kushoto) wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na Viongozi mbali mbali wa Kanisa hilo leo,[Picha na Ikulu.]10/09/2018.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na  Uongozi wa  Kanisa la Anglikana Tanzania ulioongozwa na  Askofu Mkuu wa kanisa hilo  Dkt. Maimbo  Willium Mndolwa (wa tatu kushoto) babada ya mazungumzo wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na Viongozi mbali mbali wa Kanisa hilo leo,[Picha na Ikulu.]10/09/2018.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na waumini wa dini zote hapa nchini kama Katiba inavyoelekeza.
Dk. Shein aliyasema hayo leo alipokuwa na mazungumzo na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dk. Maimbo Willium Mndolwa aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais akiwa amefuatana na viongozi wengine wa Kanisa hilo hapa Zanzibar akiwemo Askofu wa Dayosisi ya Zanzibar Michael Henry Hafidh.
Katika maelezo yake Rais Dk. alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawathamini wananchi wake wote pamoja na dini zao kwa kufahamu kuwa kuimarika kwa imani za dini zao ni kuimarika kwa amani, utulivu, uvumilivu na ustahamilivu.
Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar ina historia kubwa katika masuala ya dini zote kwani historia inaonesha kwamba katika ukanda wa Afrika ya Mashariki dini ya Ukiristo na Uislamu zilianza kuingia Zanzibar kabla ya maeneo mengine ya ukanda huo.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa ushirikiano na uhusiano mwema wa kidini hapa Zanzibar ulikuwepo tokea karne zilizopita na ndio maana Awamu zote za uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umekuwa ukiuendeleza ushirikiano huo sambamba na kufuata misingi ya Katiba katika masuala mazima ya dini.
Akizungumzia suala zima la ustahamilivu, Rais Dk. Shein alieleza kuwa katika mambo ya dini na imani ya kuabudu, Zanzibar imekuwa ikipata heshima tangu miaka iliyopita kwa kuwa ni nchi yenye ustahamilivu wa dini.
Aliongeza kuwa watu wa Zanzibar hawakuwa na mizozo na wala hawakuwa wakifarakana kwa mambo ya dini na badala yake waliishi kwa pamoja kwa kushirikiana na kupendana hali ambayo iliimarisha udugu wao wa asili walionao.
Rais Dk. Shein alisema kuwa watu wa Zanzibar wana dini mbali mbali lakini wanaishi kwa kusikilizana na kupelekea Zanzibar kujulikana kwa ustahamilivu wa dini na kuwafanya waumini kustahamiliana kama alivyoamrisha MwenyeziMungu.
Katika sifa hii ya ustahamilivu wa kidini katika mwaka 1953 zilitolewa Stempu maalum na Posta ya Zanzibar iliyoelezea mafanikio haya ambapo Msikiti, Kanisa na Temple ya Kihidni vimewekwa pamoja ili kuonesha ushirikiano, alisisitiza Dk. Shein.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alimuhakikishia kiongozi huyo wa Anglikana Tanzania kuwa ataendelea kumpa ushirikiano katika kufanikisha utendaji wake wa kazi.
Alieleza kuwa Waumini wa dini zote hapa Zanzibar wako huru kufanya ibada zao na shughuli zao za kidini na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitomuingilia mtu yoyote katika dini yake kwani inatambua na inafahamu umuhimu wa dini katika imani ya mwanaadamu.
Nae Dk. Maimbo Willium Mndolwa, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuiongoza Zanzibar kwa amani, upendo na uvumilivu na kueleza kuwa kwa niaba ya Kanisa la Anglikana wanatoa shukurani zao na kumtakia heri na Baraka katika uongozi wake.
Askofu Mndolwa alimueleza Rais Dk. Shein kuwa waumini wa Kanisa la Anglikana hapa Zanzibar wamekuwa wakivutiwa na ushirikiano mkubwa wanaoupata kutoka kwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein.
Alisisitiza kuwa kuwepo kwa amani na utulivu hapa Zanzibar kumetokana na uongozi thabiti wa Rais Dk. Shein na Serikali yake hasa ikizingatiwa kuwa kumekuwepo kwa mawasiliano mazuri na ushirikiano wa kutosha kati ya viongozi wa Kanisa hilo na uongozi wa Serikali.
Aidha, Askofu Mndolwa alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuundwa Kamati inayowashirikisha viongozi wa dini ya Kiislamu na viongozi wa dini ya Kikristo katika kusimamia amani na utulivu hapa Zanzibar.
Sambamba na hayo, uongozi huo wa kanisa Anglikana pamoja na waumini wake ulimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa  wataendelea kushirikiana na  Serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar  katika kuendeleza na kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.
Askofu Mndolwa alichaguliwa katika Sinodi (Bunge) Maalum la Kanisa Anglikana Tanzania Februari 15 mwaka 2018 na kukabidhiwa wasfa huo katika Ibada Takatifu iliyofanyika siku ya Pentekoste ya May 20, 2018 baada ya Askofu Dk. Jacob Erasto Chimeledya kumaliza muda wake wa kazi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment