ZURA yatangaza kushuka bei ya petroli, dizeli - Karafuu24 Blog

Breaking

Wednesday, 8 August 2018

ZURA yatangaza kushuka bei ya petroli, dizeli

WAKATI wafanyabiashara wa magari ya abiria (daladala) wakiomba Idara ya Usafiri na Leseni kuongeza bei ya nauli kutokana na kupanda kwa gharama ya mafuta kuanzia mwezi Julai, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), imetangaza kushuka kwa bei ya mafuta hayo kwa mwezi Agosti.

Awali madereva wa daladala walitaka serikali kuongeza bei ya nauli kutoka Sh. 300 hadi 400, ili kuenda na gharama za mafuta.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa mamlaka ya ZURA, Khuzaimat Bakar Kheir, alisema kushuka kwa gharama kunatokana na mabadiliko ya bei ya bidhaa ya mafuta kubadilika kwa wastani wa uuzaji katika soko la dunia.

Alisema licha ya kushuka kwa bei ya mafuta, lakini bado bei ya mafuta ya taa imepanda na kufikia Sh. 77 kwa lita kutoka Sh. 1,777 kwa mwezi wa Julai hadi Sh. 1,854 kwa mwezi wa Agosti, 2018.

Alisema bei ya mafuta ya petroli imeshuka kwa Sh. 25 kwa lita kutoka Sh. 2,435 ya mwezi wa Julai hadi Sh. 2,410.

Alisema mafuta ya dizeli yameshuka kwa Sh.35 kwa lita kutoka Sh. 2,430 ya mwezi wa Julai hadi Sh. 2,395.

Aidha, alisema mafuta ya meli kwa Agosti imeshuka kwa Sh.36 kwa lita kutoka Sh. 2,259 kwa mwezi wa Julai hadi Sh. 2,222 kwa Agosti.

Kadhalika bei ya mafuta ya ndege pia imeshuka kwa Sh. 20.96 kwa lita moja kutoka Sh. 1,936,73 mwezi Julai hadi Sh. 1,915.77 kwa mwezi wa Agosti.

Alisema ZURA inapanga bei kwa kuzingatia wastani wa mwenendo wa mabadiliko gharama za mafuta katika soko la dunia.

Alisema pia wanazingatia gharama za uingizaji na uhifadhi wa mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam usafirishaji hadi Zanzibar.

No comments:

Post a Comment