Rais Magufuli ‘maendeleo hayana chama, tukianza kwenda kwa vyama na makabila hatutafika’ - Karafuu24 Blog

Breaking

Wednesday, 1 August 2018

Rais Magufuli ‘maendeleo hayana chama, tukianza kwenda kwa vyama na makabila hatutafika’

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli  amesema kuwa maendeleo hayana chama wala kabila na hivyo viongozi huteuliwa kushika nafasi mbalimbali kutokana na uwezo wao wa utendaji kazi pamoja na uadilifu wao.
Rais Magufuli ameyasema  hayo leo wakati wa hafla ya uapisho wa Wakuu wa mikoa 4, Makatibu Wakuu 2, Manaibu Katibu Wakuu 2 na Makatibu Tawala wa Mikoa 13 Ikulu jijini Dar es salaam, ambapo aliwataka  viongozi hao kutekeleza vyema wajibu wao katika kuwaletea maendeleo wananchi.
“Naambiwa kuwa nimechagua wapinzani, kwa Tanzania tunayoijenga ya umoja tukianza kwenda kwa vyama na makabila hatutafika, tuchague viongozi kwa utendaji wao wa kazi”Alisema Rais Magufuli.
Aliongeza  kuwa “Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kasilikizeni wananchi na mkashughulikie kutatua matatizo ya wananchi katika maeneo yenu”
Aidha, Rais Magufuli alionesha kutofurahishwa na hali ya migogoro inayotokea katika maeneo mbalimbali nchini , ambayo inaweza kutatuliwa na viongozi wa maeneo hayo, ambapo amewataka viongozi hao kuwa chachu ya kutatua kero za wananchi.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Samia Suluhu Hassan  aliwataka viongozi hao kufanya kazi kwa bidii  na kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato na matumizi  katika halmashauri  zao.
“ Kasimamieni kiapo hiki  mlichoapa, mkawe na uhusiano mzuri na mtakao wakuta kule lakini pia nawataka mkafanye kazi sambamba na kutekeleza ilani ya  chama cha Mapinduzi” alisema Makamu wa Rais Samia
Naye, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  aliwapongeza viongozi hao walioapishwa  na kusema kuwa Rais amewaamini  na ni dalili watafanyakazi katika kutumikia taifa kwa uadilifu.
“ Anzeni kujifunza, mtakayoyakuta ofisini, jukumu lenu wote ni kusimamia kikamilifu shughuli za mbalimbali za serikali zitakazo chochea maendeleo ya wananchi  kwa ngazi zote” amesema Waziri Mkuu.
Hafla hiyo ya uapisho kwa  viongozi hao wa umma, ilihudhuriwa na viongozi mbali wakiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Suleiman Jaffo, Jaji Kiongozi Dkt. Elieza Felshi , Wakuu wa Mikoa,  viongozi wa dini pamoja na viongozi wa vyama vya  siasa.

No comments:

Post a Comment