NEC YAUJIBU UBALOZI WA MAREKANI SAKATA LA UCHAGUZI WA MARUDIO - Karafuu24 Blog

Breaking

Thursday, 16 August 2018

NEC YAUJIBU UBALOZI WA MAREKANI SAKATA LA UCHAGUZI WA MARUDIO


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekanusha taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini kwamba katika uchaguzi mdogo uliofanyika Agosti 12, mwaka huu uligubikwa na vurugu na uvunjifu wa sheria.

Aidha, tume pia imeutaka ubalozi huo kuthibitisha wanachokieleza juu ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Buyungu na kata 36.

Kwa mujibu wa taarifa ya NEC iliyotolewa na Ofisa Habari Mwandamizi wa tume hiyo, Christina Njovu, Ubalozi huo umetoa taarifa inayotoa tuhuma dhidi ya serikali, tume na jeshi la polisi kuwa sheria haikufuatwa na pia ulikuwa na vurugu katika uchaguzi huo.

“Uchaguzi mdogo huwa hauna waangalizi wa kimataifa, je ubalozi huo umetoa wapi taarifa hizo? Na hayo waliyoyaona, wameyaona kwa kutumia utaratibu upi na sheria ipi?

“Katika Jimbo la Buyungu mgombea wa ubunge mmojawapo kupitia Chadema alijitokeza kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na kueleza hisia zake na kusema bayana kuwa amekubaliana na matokeo na ameshukuru kwa kuwa uchaguzi huo umemjenga.

“Kilichotokea Arusha ni vurugu mitaani mbali na maeneo ya vituo vya kupigia kura, kwa kuwa vurugu hizo zilipelekea jinai kufanyika vyombo husika vinashughulikia.

“Aidha, tume inapenda kuufahamisha umma kuwa Tanzania ni nchi huru na inaendesha chaguzi zake kwa mujibu wa katiba yake na sheria za uchaguzi. Kama kuna ambaye hajaridhika bado sheria za nchi zinampa fursa ya kuwasilisha malalamiko yake kwenye mamlaka mbalimbali zilizopo,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.No comments:

Post a Comment