Lugola Awageukia Trafiki Waonevu - Karafuu24 Blog

Breaking

Thursday, 9 August 2018

Lugola Awageukia Trafiki Waonevu

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola, amewageukia askari wa usalama barabarani (trafiki) wanaowabambikia makosa madereva kwa lengo la kupewa rushwa, akionya kuwa siku zao zinahesabika.

Waziri Lugola alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na chombo kimoja cha habari, akifafanua malalamiko ya wananchi kuhusu trafiki kukamata magari na kuwabambikia kesi madereva.

Alisema wananchi hao wamekuwa wakiwalalamikia askari wa kikosi cha usalama barabarani kuwa wanawabambikia makosa madereva kwa lengo la kujipatia rushwa.

“Baadhi ya wananchi wanawatupia malalamiko baadhi ya askari wetu kuwa wanatumia mwanya huu ambao tumeongeza udhibiti na mikakati ya udhibiti ajali za barabarani wao wanabambikiza makosa kwa madereva kwa lengo la rushwa,” alisema.

Waziri Lugola alisema anaamini kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Simon Sirro, anaendelea kusimamia jeshi hilo na atachukua hatua stahiki.

“Nitumie fursa hii kuwaonya askari hawa, tunaletewa taarifa zingine tunazifanyia kazi na ikithibitika ni kweli tutaendelea kuchukua hatua kwa wahusika,” alisema.

“Kuna dereva ambaye alikamatwa Agosti 6, maeneo ya Vingunguti akiwa na gari aina ya Suzuki Station Wagon T 443 DHA ndani akiwa na maboksi ya taa. Alipigwa  faini kwa kosa la kupakia bidhaa kwenye siti za abiria,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Lugola alisema kwa sasa kuna mkanganyiko kama ni kweli gari hilo limetenda kosa kwa kuweka bidhaa kwenye siti za abiria au la.

“Tumefanya mawasiliano na IGP ili awatake kikosi cha usalama barabarani kijiridhisha kama nilicholalamikiwa ni cha kweli au la, ili tuone ni hatua gani zichukuliwe,” alisema.

Waziri Lugola alitumia nafasi hiyo kuwaonya askari wa usalama barabarani kuwa wasijaribu kujihusisha na vitendo vya rushwa kwenye serikali ya awamu ya tano kwa kuwa kufanya hivyo watakuwa wanahatarisha kazi zao.

“Tumeshawaambia mara kwa mara kwamba nafasi hii haipo tena mwanya huo wasiutumie watapata matatizo kama si kupata tabu sana, kwa hiyo waendelee kuchapa kazi na kudhibiti ajali na wale wanaofanya kazi vizuri tunawapa moyo waendelee,” alisema.

Februari mwaka huu, askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, ambaye video ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ilimwonyesha akichukua rushwa ya Sh. 5,000, alifukuzwa kazi kwa kulifedhehesha Jeshi la Polisi.

Video hiyo ambayo ilianza kusambaa kwenye makundi mbalimbali ya kijamii kama WhatsApp na Facebook ilimwonyesha askari huyo akipokea kiasi hicho cha fedha iliyoambatanishwa na leseni eneo la Mwenge, Dar es Salaam.

Katika tukio hilo ya dereva mmoja aliyeombwa rushwa alimrekodi askari huyo kupitia simu yake ya mkononi wakati akimpatia rushwa hiyo iliyowekwa chini ya leseni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jumanne Murilo, aliiambia Nipashe wakati huo kuwa tayari askari huyo ameshachukuliwa hatua kwa kufukuzwa kazi.

Kamanda Murilo alisema askari huyo hadi anafukuzwa kazi ndani ya Jeshi la Polisi alikuwa amefanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.

“Tukio hili lilifanyika eneo la Mwenge na baada ya kulibaini tulianza uchunguzi wetu ambao juzi ulikamilika na kubaini tukio hilo lilikuwa la kweli amepokea rushwa hivyo tumemuondoa kazini,” alisema.

Vitendo vya kuwachukua video trafiki wanaopokea rushwa vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara, ambapo tukio lingine linalofanana na hilo lilitokea mkoani Tanga mwaka 2015.

Katika tukio hilo, aliyekuwa askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Koplo Anthony Temu, mwenye namba F785, alifukuzwa kazi kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa.

Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zuberi Mwombeji, ambaye alisema lilitokea barabara kuu ya Chalinze-Segera.

Alisema kupitia mitandao ya kijamii askari huyo alionekana akipokea rushwa kutoka kwa dereva wa gari alilokuwa amelisimamisha kwa ajili ya kukagua makosa yanayoweza kuhatarisha usalama barabarani.

Tukio lingine ni lile lililotokea visiwani Zanzibar mwaka uliopita, baada ya Sajini Hamad Kassim wa Kituo cha Mkokotoni visiwani humo, kuonekana kwenye video akipokea rushwa ya Sh. 10,000.

Rushwa hiyo aliiomba kutoka kwa raia wa kigeni baada ya kumkamata akiwa hajafunga mkanda wakati akiendesha gari.

No comments:

Post a Comment