BALOZI SEIF ALLI IDDI ATEMBELEA KWENYE MAONYESHO YA NANE NANE MOROGORO. - Karafuu24 Blog

Breaking

Thursday, 9 August 2018

BALOZI SEIF ALLI IDDI ATEMBELEA KWENYE MAONYESHO YA NANE NANE MOROGORO.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema umefika sasa kwa kwa Wizara na Taasisi zinazohusika na Sekta ya Elimu Nchini kumuandaa Mwanafunzi katika masomo ya Kilimo kuanzia ngazi ya Msingi hadi Sekondari ili atakapofikia uwezo wa kuingia chuo Kikuu awe tayari ameshaelewa nini Kilimo.
Alisema uingizwaji wa  Mitaala ya Kilimo ndani ya masomo ya kawaida maskulini itamuwezesha Wanafunzi kujitayarisha mapema katika muelekeo wa kujijengea uwezo wa ajira ya uhakika ndani ya Sekta ya Kilimo wakati amalizapo masomo yake ili aweze kujitegemea kupitia Sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa Taifa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa ushauri wakati akizungumza na vyombo mbali mbali vya Habari mara  baada ya kumaliza ziara yake ya kuangalia Maonyesho  mbali mbali ya Siku ya Nane Nane yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoani Morogoro.
Alisema wakati Nchi imelenga kuwa Taifa la Viwanda litakayokuwa na Uchumi wa Kati ifikapo Mwaka 2525 maandalizi ya haraka yanahitajika yatakayokwenda sambamba na mpango huo utakaotoa afueni ya changamoto ya ajira inayowakumba zaidi Vijana wanaomaliza masomo yao ya Sekondari na Vyuo.
“ Mwanafunzi lazima aandaliwe mapema tokea elimu ya Msingi na Sekondari ili afikapo chuo Kikuu awe tayari ameshaelewa nini hasa Kilimo”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif aliwaeleza Wanahabari hao kwamba Wanafunzi wanaweza kuwa wajasiriamali wakubwa endapo wataamua kuelekeza nguvu zao katika Kilimo kilichoonyesha mabadiliko makubwa kutokana na Utaalamu wa kisasa unaotumika kwenye Sekta hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwasihi Vijana wa Zanzibar na Tanzania Bara kwa jumla kujikita zaidi katika Sekta ya kilimo huku Sewrikali zote mbili zikiendelea kujikita katika kutilia mkazo Sekta hiyo kwa kuongeza miundombinu imara zaidi inayokwenda na wakati wa sasa wa sayansi na Teknolojia.
Mapema Naye Katibu Tawala msaidizi wa Mkoa wa Morogoro  anayesimamia Kilimo, Uchumi na Uzalishaji Bwana Ernest Mkango alisema Maonyesho hayo yameshirikisha Taasisi na Wajasiri Amali kutoka Mikoa ya Tanga, Dar es salaam, Pwani na wenyeji Morogoro.
Bwana Ernest  alisema juhudi kubwa zimeanza kuchukuliwa na Serikali Kuu katika kuimarisha  miundombinu ya Sekta ya Kilimo sambamba na  upatikanaji wa zana bora na za kisasa za Kilimo zitakazowashawishi moja kwa moja Vijana kujiingiza katika Sekta ya Kilimo.
Katibu Tawala huyo Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro alifahamisha kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana kutoka kwa Washirika wa Maonyesho hayo kutokana na ubinifu wa hali ya juu ulitumika katika uzalishaji wa Bidhaa na Mazao tofauti yanayoonekana kupendwa na Wananchi wanaotembelea maonyesho hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kutembelea baadhi ya Mabanda ya Maonyesho yao ikiwa ni pamoja na Manispaa ya Kiondoni Jijini Dar es salaam pamoja na Banda la Halmashauri ya Mkuranga.
Nyengine ni Banda la Manispaa ya Tanga, Halmashauri ya Kilosa Morogoro,Mradi wa kilimo cha mboga mboga wa Kanisa la Anglican Dayosisi ya Morogoro, Kiwanda cha Sukari Morogoro pamoja na Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro.
Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amewapongeza Wajasiri Amali Nchini kwa hatua kubwa waliyopiga katika uzalishaji wa Bidhaa zinazokwenda na soko linalokubalika Kitaifa na nyengine Kimataifa.
Maadhimisho ya Siku ya Nane Nane  yafikia kilele chake Jumatano Tarehe 8 Agosti ambayo huadhimishwa Nchini Kote na ni siku inayokuwa mapumziko Tanzania Nzima.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akivishwa Skafu na Vijana Chipukizi wa Morogoro mara alipoingia kwenye Unjwa wa Maonyesho wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kiondoni Bwana Hija Saleh akimpatia maelezo Balozi Seif alipotembelea Banda la Manispaa hiyo kwenye Maonyesho ya Nane Nane Morogoro.
Hiba ya Kitalu cha Manispaa ya Kinondoni kinavyoonekana kikiwa katika hali ya kupendeza ndani ya Uwanja wa Maonyesho ya Nane Nane Morogoro.
Balozi Seif  akiendelea na ziara yake ya kulikagua Banda la Maonyesho la Halmashauri ya Mkuranga liliomo ndani ya Uwanja wa Maonyesho wa Mwalimu Julius K. Nyerere Morogoro.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akifurahia na kuridhika na vidhaa zinazotengenezwa na Mjasiri Amali wa Mkoa wa Tanga, Jina halikupatikana.
Balozi Seif akinunua moja ya bidhaa zilizotengenezwa na Kikundi cha Wajasiri Amali kutoka Mkoani Tanga kwenye Maonyesho ya Nane Nane Morogoro.
Moja ya Kitalu cha zao la tungule likionekana kupendeza kutokana na Utaalamu mkubwa uliotumika kwenye ukulima wake ndani ya Uwanja wa Maonyesho Mkoani Morogoro.
Moja ya Bwana la kufugia Samaki la Chuo Kikuu cha sokoni Mkoani Morogoro ambalo Balozi Seif na Ujumbe wake alipata muda wa kulitembelea.
Balozi Seif akifurahia Ukulima wa Mpunga uliooteshwa katika mfumo wa Taaluma ya kisasa kwenye Kitalu cha Kanisa la Anglican Dayosisi ya Morogoro kiliomo ndani ya Maonyesho ya Nane Nane.
Balozi Seif  akiendelea na ziara yake ya kukagua mambo mbali mbali ndani ya Uwanja wa Maonyesho wa Nane Nane wa Mwalimu Julius K. Nyerere Mkoani Morogo.
Balozi Seif akimshangaa Panya aliyepewa mafunzo maalum kuchunguza na hatimae kugundua  miripuko ya Mabomu ndani ya Banda la Chuo Kikuu cha Sokoine Mkoani Morogoro.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na vyombo mbali mbali vya Habari mara baada ya kumaliza zaiara yake ya kutembelea mabanda mbali mbali ndani ya Uwanja wa Mwalim Julius K. Nyerere Mkoani Morogoro.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Frais wa Zanzibar
07/08/2018.

No comments:

Post a Comment