Baada ya Ajali ya Kingwangala, Lugola awageukia Madereva wa Serikali..Adai Ndio Vinara wa Kuvunja Sheria - Karafuu24 Blog

Breaking

Sunday, 5 August 2018

Baada ya Ajali ya Kingwangala, Lugola awageukia Madereva wa Serikali..Adai Ndio Vinara wa Kuvunja Sheria

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola, ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kuwachukulia hatua kali viongozi wa serikali pamoja na madereva wao wanapovunja sheria za usalama barabarani.

Amesema madereva wa viongozi wa serikali wamekuwa vinara kwa uvunjaji Sheria za Usalama barabarani na kulitaka Jeshi hilo liwashughulikie bila kuangalia vyeo walivyo navyo.

Alitoa agizo hilo jana wakati akizindua rasmi Baraza jipya la Taifa la Usalama Barabarani jijini hapa.

Akionyesha kukerwa na ajali hizo, alisema takwimu za Jeshi la Polisi nchini zinaonyesha kuwa madereva wa viongozi wa serikali wamekuwa wakiongoza katika matukio ya uvunjaji wa Sheria za Usalama Barabarani kwa kiwango cha juu.

Pia madereva hao wamekuwa wakilalamikiwa kwa kuendesha mwendo kasi kinyume na sheria huku viongozi wao wakikaa kimyaa bila kuwaonya.

"Kiongozi ambaye dereva wake atabainika kuendesha kinyume cha sheria zetu za nchi achukuliwe hatua stahiki kama ilivyo kwa madereva wengine bila kujali anamwendesha bosi gani," alionya Lugola.

Aidha, aliwataka viongozi mbalimbali wa serikali kuwa mfano katika kusimamia sheria za nchi kwa kuendesha kwa tahadhari ili kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikitokea kutokana na mwendo kasi.

"Sheria imewekwa ili kumlinda kila raia na ndiyo maana leo hii mtu akinywa sumu na akanusurika kufa anashtakiwa, hivyo basi kama wewe kiongozi upo na dereva wako anasababisha ajali kizembe atachukuliwa hatua kali kama ilivyo kwa watu wengine bila kumwonea huruma," alisema.

Alisema Sheria ya Usalama Barabarani inatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kutoa adhabu kali ambayo madereva wengi watawajibishwa na kupunguza ajali za kizembe.

"Hivi sasa mtu anaposababisha ajali anakuwa na shauku sana ya kufikishwa mahakamani. Hii yote ni kwasababu ya kile ambacho atakikuta huko, akifikishwa mahakamani na akakiri kosa anapewa faini ambayo ni ndogo ukilinganisha na ajali aliyosababisha," alisema Lugola.

Aidha, alisema Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani wapo katika operesheni ya ukaguzi wa leseni kwa watu ambao walipatiwa bila ya kwenda shule na watakao bainika watafutiwa umiliki.

"Kuna watu walipatia leseni mezani sasa ni muda mwafaka wa kufanya ukaguzi kama ambavyo Rais Magufuli alivyokagua watumishi wasio na vyeti na sisi tunakagua walio na leseni bila vyeti na watakao bainika tutazifungia leseni zao," alisema.

Hata hivyo, alilitaka Jeshi la Polisi nchini kuongeza umakini katika kusimamia Sheria za Usalama Barabarani ili kukomesha ajali zinazotokea mara kwa mara nchini.

Naye Mjumbe wa Baraza hilo la Usalama Barabarani, Hamza Kasongo, alisema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali watahakikisha wanaanza kumaliza tatizo la ajali za barabarani hasa kwa magari ya serikali.

"Madereva wetu wakiwa wanaendesha STK au STL huwa wananajiona wao ni watu maalumu sana na kuvunja sheria za usalama barabarani kwa kuendesha ovyo na kupita kwa mwendo kasi hata maeneo wasiyo ruhusiwa kufanya hivyo, sasa ndiyo tutaanza nao kwa kuwashughulikia," alisema Kasongo.

No comments:

Post a Comment