Watumishi TTCL mbaroni udukuzi taarifa za serikali - Karafuu24 Blog

Breaking

Wednesday, 25 July 2018

Watumishi TTCL mbaroni udukuzi taarifa za serikali

WAFANYAKAZI wawili wa Kampuni ya Mawasiliano ya TTCL wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kwa tuhuma za kufanya udukuzi wa data za taasisi za serikali kupitia TTCL na kuziuza.

Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa aliwataja jana wafanyakazi hao kuwa ni Kelvin Siame (25) wa kitengo cha Huduma kwa Wateja TTCL mkazi wa Tabata Segerea na Mhasibu wa TTCL Lilian Hosea (36) mkazi wa Mbezi Beach.

Alisema wafanyakazi hao wamekuwa wakiihujumu kampuni hiyo kwa kufanya udukuzi wa data mbalimbali na hadi sasa wameisababishia hasara ya Sh. Milioni 45 kampuni hiyo.

Kamanda Mambosasa alisema Julai 12, Jeshi la Polisi lilipata taarifa kutoka kwa Ofisa Upelelezi wa TTCL kuwa, kuna wafanyakazi wa shirika hilo wanajihusisha na udukuzi wa data za kampuni ya TTCL kutoka taasisi za serikali zinazotumia mtandao wa TTCL.

“Taasisi hizi ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kamanda Mambosasa alisema taasisi hizo zimekuwa zikinunua data kutoka kampuni ya TTCL kwa ajili ya matumizi ya kila siku.

Alisema watuhumiwa hao wamekuwa wakiiba data hizo na kuwauzia watumiaji binafsi kwa manufaa yao na kulisababishia shirika hasara ya Sh. milioni 46 hadi sasa.

“Tumewahoji na wamekiri kushirikiana na baadhi ya mawakala wa TTCL kuuza data ambazo walikuwa wakizidukua kutoka kwenye taasisi hizi, baada ya upelelezi kukamilika tutawafikisha mahakamani,” alisema.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mambosasa amewatahadharisha wananchi kuhusu ujumbe mfupi kutoka kwa matapeli unaoeleza kuwa wameshinda fedha katika droo ya bahati nasibu wakati siyo kweli.

“Matapeli hawa wamekuwa wakiwataka watu watume kianzio cha fedha kama bima ili kupata zawadi ya fedha walizoshinda. Taratibu za bahati nasibu wachezaji hawatakiwi kulipa kiasi chochote cha fedha kama utangulizi ili kupata zawadi ya ushindi. Yoyote atakayepokea ujumbe wa aina hii watoe taarifa polisi ili ziweze kufanyiwa kazi,” alisema.

No comments:

Post a Comment