Lugola: Siko tayari kutumbuliwa - Karafuu24 Blog

Breaking

Friday, 27 July 2018

Lugola: Siko tayari kutumbuliwa


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amevionya vyama vya siasa kwa kusema hayuko tayari kutumbuliwa kwa sababu ya kushuhudia mtu yeyote akitoa lugha za kichochezi kwa kisingizio cha kumnadi mgombea jukwaani.

Lugola ametoa onyo hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma ambapo amesema kuwa  mgombea atakayetoa matamshi ya uchochezi atakamatwa na huenda akakosa haki ya kuendelea na uchaguzi.

 “Siko tayari kutumbuliwa ila niko tayari kuwatoa matumbo wote watakaokuwa wanajihusisha na uchochezi kabla tumbo langu halijatumbuliwa, navionya vyama vyote vya siasa, mtu yoyote wa chama chochote cha siasa atakayeonekana akitumia kinywa chake kutoa matamko ambayo ni ya uchochezi ajue kwamba hayuko salama”, amesema Lugola.

Waziri Lugola ameongeza kuwa hayuko tayari kumuangusha Rais kwani katika kiapo chake, wakati anaapishwa aliahidi kuwalinda watanzania, kudumisha amani na usalama.

Kauli hiyo ya kuvionya vyama vya siasa imekuja wakati vyama hivyo vipo kwenye kampeni ya uchaguzi mdogo wa madiwani na ubunge, utakaofanyika Agosti 12 tarehe iliyopangwa na tume ya taifa ya uchaguzi (NEC) ili kujaza nafasi zilizowazi katika Jimbo la Buyugu na kata 79 Tanzania bara na Visiwani.

No comments:

Post a Comment