Kangi Lugola Awatoa Hofu Raia wa Msumbiji - Karafuu24 Blog

Breaking

Thursday, 19 July 2018

Kangi Lugola Awatoa Hofu Raia wa Msumbiji

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewatoa hofu na kuwahakikishia raia wa Msumbiji waliokimbilia nchini kwa madai ya kuwapo machafuko nchini humo kuwa wako salama, huku taratibu za kuhakikisha wanarejea kwao zikiendelea.

Lugola alitoa kauli hiyo jana alipowatembelelea raia hao katika Kijiji cha Kivava Wilaya ya Mtwara mkoani hapa kwa lengo la kuwajulia hali kutokana na mazingira hayo.

Waliokimbilia nchini wamefikia 646 ambapo raia wa Msumbiji ni 102 pamoja na Watanzania wanaofanya shughuli zao nchini humo ni 544.

Alisema raia hao waondokane na dhana ya kujiona kuwa wao ni wakimbizi, akisema nchini kwao hakuna machafuko bali ni kikundi cha watu wachache ambao wameamua kufanya vurugu na kusababisha hali ya taharuki kwa wananchi.

Raia hao wanapatiwa huduma zote muhimu za kibinadamu na serikali ya Tanzania yakiwamo malazi, chakula, afya hadi hapo taratibu za kuwarejesha kwao zitakapokamilika.

Lugola alisema taratibu hizo zimefikia mahali pazuri kutokana na mawasiliano yanayoendelea kati ya serikali ya Tanzania na Msumbiji.

“Tunawahakikishia mpo katika hali ya amani na salama hadi hapo mtakaporejea nchini kwenu. Muwe na amani msiwe wanyonge na hapa mlipo siyo kambini, bali ni sehemu ya hifadhi tu na ninyi siyo wakimbizi. “Ila ni mambo yametokea nchini kwenu ndipo mkaona mkimbilie nchi jirani.”

Aliagiza zoezi la kuwarudisha kwao lisichukue zaidi ya siku tatu na kwamba kuanzia jana liwe limekamilika, ili wajereshwe kwao na  kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Suzan Kolimba, alisema wao kama wizara watahakikisha wanadumisha mahusiano baina ya nchini hizo mbili.

No comments:

Post a Comment