CCM Z'BAR YAZUNGUMZA NA WANAFUNZI WALIOFAULU KIDATO CHA SITA - Karafuu24 Blog

Breaking

Monday, 23 July 2018

CCM Z'BAR YAZUNGUMZA NA WANAFUNZI WALIOFAULU KIDATO CHA SITA

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewapongeza wanafunzi waliofaulu mtihani wa taifa wa kidato cha sita mwaka 2018, kwa kupata daraja la kwanza, pili na tatu (Division I,II&III).
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya siasa na uhusiano wa kimataifa CCM Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa  Mwl. Kombo Hassan Juma,  alipokutana na wanafunzi 450 waliofaulu mtihani huo kwa upande wa Unguja, huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.
Mwl. Kombo alisema Chama Cha Mapinduzi kinawapongeza wanafunzi hao kwa juhudi zao za kusoma kwa bidii hadi wakafaulu mtihani huo.
Alieleza kwamba licha ya CCM kuwa taasisi ya kisiasa bado ina jukumu la msingi la kufuatilia,kuhakiki na kutathimini mwenendo wa hali ya elimu nchini.
Alieleza kwamba maendeleo ya nchi yoyote duniani yanatokana na fikra na ubunifu wa wasomi wa fani mbali mbali zinazosaidia kuharakisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya nchi.
Mwl. Kombo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya ajira, elimu na mafunzo Afisi kuu CCM Zanzibar aliwambia wanafunzi hao kwamba CCM itaendelea kuwaunga mkono katika safari yao ya kielimu ili waweze kuhitimu elimu ya juu na kuwa wataalam watakaoitumikia nchi kwa uadilifu.
“ Wazee na walezi sote tunatakiwa kuwajibika  katika kusimamia na kuwalea katika maadili mema vijana wetu ili waweze kujifunza na kusoma kwa bidii na kufaulu vizuri katika mitihani mbali mbali ya kitaifa.
Serikali zote mbili ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania na Zanzibar zinaendelea kuimarisha sekta ya elimu hasa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi waliofaulu kujiunga na Vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu.”, alisema Mwenyekiti huyo na kuwasisitiza wanafunzi nchini kusoma kwa bidii ili wanufaike na fursa hiyo.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Laila Burhan Ngozi aliwashauri wanafunzi mbali mbali wa ngazi za sekondari nchini kuepuka vikundi viovu badala yake wasome kwa bidii kwa lengo la kuwa na umahiri wa kumudu masomo ya Chuo kikuu.
Pia aliwasihi wanafunzi ambao viwango vyao vya ufaulu havikukidhi vigezo vya kuendelea na elimu ya juu wasikate tamaa bali wajiendeleze kitaaluma na kuweza kukamilisha malengo yao waliojiwekea.


Katika kikao hicho pia waliudhuria wanafunzi wawili wa Zanzibar waliofanya vizuri zaidi katika mtihani wa kidato cha Sita mwaka huu, ambao ni Ndugu Biubwa Khamis Ussi kutoka shule ya Sekondari ya SOS na Ndugu Fahad Rashid Salum kutoka Shule ya Sekondari Lumumba.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya siasa na uhusiano wa kimataifa CCM Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa  Mwl. Kombo Hassan Juma, akizungumza na wanafunzi wa kidato cha Sita Unguja waliofaulu mtihani mtihani wa taifa daraja la kwanza hadi la tatu.
WANAFUNZI wa kidato cha Sita waliofaulu mtihani wa taifa mwaka 2018, wakisikiliza kwa makini nasaha za viongozi mbali mbali wa CCM katika Kikao cha kuwapongeza kilichofanyika Afisi Kuu CCM, Kisiwandui Zanzibar.
                                            MWISHO

No comments:

Post a Comment