BALOZI SEIF ALLI IDDI AFANYA ZIARA KATIKA HOSPITALI YA MNAZI MKOJA - Karafuu24 Blog

Breaking

Tuesday, 24 July 2018

BALOZI SEIF ALLI IDDI AFANYA ZIARA KATIKA HOSPITALI YA MNAZI MKOJA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kutowavunja moyo Watendaji wake  pale wanapolalamikia haki na maslahi yao pamoja na vitendea kazi jambo linaloweza kusababisha uwajibikaji mbovu katika kuwahudumia Wagonjwa.
Alisema tabia ya dharau  na kibri  wakati mwengine ambazo huonyeshwa na  baadhi ya Viongozi wanaosimamia Maslahi ya Watendaji huchangia uwajibikaji mbovu unaoleta kero na hatimae kuwaaudhi Wananchi wanaohitaji huduma za Afya.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipofanya ziara fupi kukagua vitengo mbali mbali vilivyomo ndani ya Majengo ya Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja  kujionea hali halisi ya uwajibikaji pamoja na kupokea changamoto zinazowakwaza Watendaji wa Hospitali hiyo.
Alisema ucheleweshwaji wa maslahi na vitendea kazi kwa watendaji hao ndio chimbuko linalozaa ushawishi unaowafanya baadhi yao kutotekeleza vyema majukumu yao na matokeo yake  Wagonjwa wanaokwenda  kupata huduma za Afya Hospitalini hapo wanakosa  imani kwa watendaji hao.
Alisema watendaji wa huduma za Afya wakati wote ni lazima wawe na furaha na kuondokana na kinyongo katika utekelezaji wa kazi zao licha ya kula kiapo cha utii na uaminifu wakati wanapojiandaa kuwatumikia vyema wagonjwa wao mara wamalizapo mafunzo yao.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuipa umuhimu wa pekee Sekta ya Afya imelazimika kuiongezea Bajeti Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja katika lengo lake la kuona huduma zinazopatikana katika Hospitali hiyo zinawaridhisha Wananchi.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliukumbusha Uongozi huo wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kuzingatia vipaumbele  katika upatikanajji wa vitendea kazi kwenye Bajeti yao ya Mwaka ili matatizo madogo madogo yaliyomo ndani ya Taasisi za Wizara ya Afya yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mapema baadhi ya Wakuu wa Vitengo tofauti vya Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja walisema  kuharibika kwa baadhi ya Vifaa muhimu vya uchunguzi wa Afya kwenye Hospitali  hiyo, mbali ya kuleta usumbufu kwa wagonjwa lakini pia husababisha kuharibika kwa mfumo wao wa kazi.
Walisema pia ucheleweshwaji wa posho, upungufu wa Hewa ya Oxygen hasa katika kitengo cha Wagonjwa wa dharura pamoja na Uhaba wa watendaji katika Wodi ya Waoto wadogo ni masuala yanayowapa wakati mgumu  katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Ali Salim Ali alisema Hospitali hiyo hivi sasa imeimarisha zaidi Kitengo cha  X ray katika azma yake ya kuwarahisishia  kazi Madaktari kwenye huduma zao za  Upasuaji.
Dr. Ali Salim alisema zipo Mashine Nne mpya zilizoagizwa kwa lengo la kuongeza nguvu katika Kitengo hicho zinazokwenda sambamba na baadhi ya watendaji wa Kitengo hicho kwa sasa wanaendelea kumalizia mafunzo yao Nchini China.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika ziara hiyo alipata fursa ya kutembelea Kitengo cha Maabara, Kitengo cha uchunguzi wa Matatizo ya Matumbo{ Utra sound}, Chumba cha Upasuaji pamoja na Wodi ya Watoto iliyoko katika Jengo Jipya la Hospitali hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulia akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Maabara Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Rashid Soud wakati alipofanya ziara fupi Hospitalini hapo.
Mkuu wa Kitengo cha Wagonjwa dharura Dr. Rashid  Hassan akimueleza Balozi Seif  majukumu wanayotekeleza wakati wa kupokea Wagonjwa Mahatuti.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mwenye Miwani akimjuilia hali Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji Khamis aliyelazwa kwa ajili ya kupatiwa huduma za Afya katika Hospitali Kuu ya Mazi Mmoja.

WA kwanza kutoka Kushoto ni Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Ngwali, Naibu Waziri wa Afya Mh. Harus Said Suleiman na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Bibi Marina Thomas.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/07/2018.

No comments:

Post a Comment