ZECO kulipa deni Tanesco - Karafuu24 Blog

Breaking

Friday, 22 June 2018

ZECO kulipa deni Tanesco


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  (SMZ), imesema itaendelea kulipa deni linalodaiwa na Shirika la Umeme Nchini (Tanesco).

Deni hilo linatokana na ununuzi wa umeme unaofanywa na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco).

Hayo yalielezwa juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Khalid Salum Muhammed, wakati akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 katika kikao cha Baraza la Wawakilishi.

Alisema kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha Zeco inalipa kwa ukamilifu ankara zake zote mpya kwa bei iliyokubaliana na pande mbili za Muungano ili kuzuia kurundikana zaidi kwa deni hilo.

“Nilieleza pia hatua ambazo serikali na Zeco zitachukua kumaliza kiasi kilichokuwa kimebaki  na kwamba inaendelea kulipa kwa ukamilifu ankara zote ili kuepuka kuingiwa deni jipya, ” alisema Dk Khalid.

Aidha, alisema  tayari Zeco imeshalipa jumla ya Sh.bilioni 18.5 na hivyo kufanya jumla ya deni lililolipwa kufikia Sh.bilioni 23.8.

Alisema serikali ya Zanzibar imelipa jumla ya Sh.bilioni mbili na kwa hivyo kufanya jumla ya malipo kwa kipindi cha miaka miwili kufikia Sh. Bilioni 15.

Alieleza kuwa kwa mantiki hiyo Zeco na serikali ya Zanzibar kwa pamoja wameshalipa Sh. Bilioni 38.8 na kubakisha deni la Sh. Bilioni 26.8.

“Itakumbukwa pia ili kulimaliza haraka deni hilo SMZ imependekeza kwa Wizara ya Fedha na Mipango  ya Zanzibar kuilipa Tanesco moja kwa moja Sh.Bilioni 18 inazoidai kupitia katika kodi ya mapato ya wafanyakazi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaofanya kazi Zanzibar ambazo hazijalipwa hapo kabla,” alisema.

Waziri huyo alisema kwa upande mwingine taasisi kadhaa za serikali ya muungano zinadaiwa na Zeco jumla ya Sh. Bilioni 1.7 ambapo itafanya jumla ya deni  la linalodaiwa kufikia Sh. Bilioni 19,7 ambazo kama zitalipwa Tanesco, itabakiza deni la Sh. Bilioni 7.1.

Hata hivyo, alisema kwa nia njema ya kumaliza deni hilo serikali ya Zanzibar ilipendekeza kwa serikali ya Muungano kulimaliza deni hilo kupitia katika madeni ya marejesho ya kodi ambayo Zanzibar inadai.

Alieleza kuwa mapendekezo hayo yalikubaliwa na yatasaidia katika maeneo mbalimbali ikiwemo kumaliza deni lote kwa mkupuo mmoja na kupunguza athari za kibajeti kwa SMZ.

No comments:

Post a Comment