ZANZIBAR YAKUBALI MUALIKO WA KUSHIRIKI MAONESHO YA KIMATAIFA YA BISHARA YATAKAYOFANYIKA CHINA. - Karafuu24 Blog

Breaking

Wednesday, 20 June 2018

ZANZIBAR YAKUBALI MUALIKO WA KUSHIRIKI MAONESHO YA KIMATAIFA YA BISHARA YATAKAYOFANYIKA CHINA.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Tanzania imekubali na kuridhia mualiko wa Kushiriki Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara uliotolewa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China yanayotarajiwa kufanyika miezi michache ijayo Katika Jimbo la Guang Zhou.
Alisema mkusanyiko wa Washiriki wa Maonyesho hayo yanayotarajiwa kuanza mnamo Tarehe 12 hadi 15 Septemba Mwaka huu wa 2018 utatoa fursa kwa Wafanyabiashara, Wawekezaji na Makampuni shiriki kubadilishana mawazo yatakayosaidia kuimarisha uhusiano baina ya Mataifa Rafiki.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akipokea Taarifa ya uthibitisho wa  Mualiko huo kutoka kwa Balozi Mdogo wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Shiaolon hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema uhusiano wa Kiuchumi, Kibiashara na hata ule wa Kisiasa baina ya Nchi  na Nchi au Taasisi na Makampuni tofauti ya Kimataifa huimarika na kukomaa zaidi iwapo wadau wa masuala hayo watajenga utamaduni wa kukutana mara kwa mara kupitia Maonyesho na Mikutano mbali mbali.
Balozi Seif ameipongeza China kwa jitihada zake za kuandaa maonyesho mbali mbali ya Kimataifa na kutoa mialiko kwa Mataifa rafiki hasa yale ya Bara la Afrika katika azma yake ya kusaidia kuunga mkono Mataifa hayo katika masuala ya kuimarisha Uchumi.
Mapema Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar  Bwana Xie Shiaolon alisema Ujumbe wa Viongozi wa Sekriterieti ya Maonyesho hayo tayari umeshafika Tanzania hivi karibuni kutoa mualiko wa kushiriki kwenye Maonyesho hayo ya Mwezi wa Septemba.
Balozi Xie Shiaolon alisema Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Guang Zhou {China - Expo }yamelenga kuongeza uhusiano wa karibu kati ya Jamuhuri ya Watu wa China na Mataifa Rafiki.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Shiaolon  aliyekaa kati kati mazungumzo yaliyofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bwana Xie Shiaolon mara baada ya mazungumzo yao kuhusu masuala ya maonyesho ya Biashara Nchini China.

Na  
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment