ZANZIBAR KUENDELEA KUIMARISHA USALAMA WA AFYA YA JAMII - Karafuu24 Blog

Breaking

Tuesday, 19 June 2018

ZANZIBAR KUENDELEA KUIMARISHA USALAMA WA AFYA YA JAMII

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed amesema Zanzibar itaendelea kutoa mashirikiano na utaalamu kwa taasisi za ndani na nje ya ya Zanzibar ili kuona utekelezaji wa mapango wa miaka mitano wa kuimarisha usalama wa afya ya jamii unafanikiwa.

Amesema kufanikiwa kwa mpango huo ni kutekeleza malengo ya Serikali ya kuwalinda wananchi dhidi ya maradhi na kujitaarisha kukabiliana na vitisho vya  afya ya jamii, miripuko ya maradhi na majanga mengine ya kimaumbile.

Waziri Hamad ameeleza hayo alipokuwa akifungua warsha ya siku tano ya kutia thamani mpango kazi wa miaka mitano wa kuimarisha usalama wa afya ya jamii Zanzibar inayofanyika Hoteli ya Golden Tulip Malindi.

Amesema Zanzibar inaendeleza  mpango huo ikiwa ni kutekeleza kanuni za Kimataifa ambapo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinawajibu wa kuhakikisha zinajenga uwezo  katika kuchunguza, kuzuia na kukabiliana kwa haraka hatari za afya ya jamii kitaifa, kikanda na kimatifa.

Aliwaeleza washiriki wa warsha hiyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuhusu mpango huo ikiwemo kupeleka madaraka ya usimamizi wa shughuli za afya ya msingi na mazingira Wilayani na kutayarisha sera na miongozo juu ya mpango huo.

Hata hivyo alibainisha kuwa mwaka jana Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ilifanya zoezi la kutathminiI uwezo wa kutekeleza sheria za afya na kugundua kunahitaji kuimarishwa mfumo uliopo wa mawasiliano, kuimarisha udhibiti wa maradhi, taratibu za uendeshaji wa huduma za dharura na kuimarisha vifaa na wafanyakazi wa dharura wenye utaalamu.

Akizungumza katika warsha hiyo Ofisa wa WHO kutoka Ofisi kuu Dar es salaam Dkt. Grace Saguti alisema lengo la mpango huo ni kujipanga na kujiandaa kwa hali na mali ili kuweza kupambana na maradhi ya mripuko na majanga yanapotokea.

Alisema mpango huo unaohitaji ushirikiano wa taasisi mbali mbali utasaidia kugundua mapema dalili za maradhi na majanga kabla ya kutokea na  kujiandaa kwa vifaa na kinga.

Mratibu wa utekelezaji wa kanuni za afya Juma Mohamed Juma alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa katika masuala ya chanjo ingawa bado haijafikia ngazi ya  kimataifa na hiyo ni miongoni mwa hatua za utekelezaji wa mpango wa afya jamii.
Ofisa wa WHO kutoka Ofisi ya Dar es salaam Dkt.Grace Saguti akitoa maelezo juu ya mpango wa miaka mitano wa kuimarisha afya ya jamii kwenye warsha iliyofanyika Hoteli ya Golden Tulip, Malindi Mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akifungua warsha ya siku tano ya mpango kazi wa kuimarisha  usalama wa afya ya jamii Zanzibar inayofanyika Hoteli ya Golden Tulip, Malindi Mjini Zanzibar.
Washiriki wa warsha ya kuimarisha afya ya jamii Zanzibar wakimsikiliza waziri wa afya (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo inayofanyika Hoteli ya Golden Tulip, Malindi Mjini Zanzibar.
Mwakilishi wa WHO Kanda ya Afirka Antonio Oke akitoa tathmini ya mpango kazi wa utekelezaji wa kuimarisha afya ya jamii katika warsha inayofanyika Hoteli ya Golden Tulip Malindi Mjini Zanzibar.

NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment