Yussuf Poulsen: Mtoto wa Baharia wa Tanga Aliyepuuzwa Tanzania, Sasa Anaing'arisha Denmark Kombe la Dunia - Karafuu24 Blog

Breaking

Sunday, 17 June 2018

Yussuf Poulsen: Mtoto wa Baharia wa Tanga Aliyepuuzwa Tanzania, Sasa Anaing'arisha Denmark Kombe la Dunia

DENMARK imeanza vyema Fainali za Kombe la Dunia baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Peru katika mchezo wa Kundi C Uwanja wa Mordovia Arena mjini Saransk Jumamosi.
Shukrani kwake mfungaji wa bao hilo pekee, mshambuliaji Yussuf Yurary Poulsen aliyetikisa nyavu dakika ya 59, siku ambayo Christian Cueva alianza kwa kuikosesha bao Peru baada ya kukosa penalti.

Yussuf Yurary Poulsen aliyezaliwa Juni 15, mwaka 1994 ni mchezaji mwenye asili ya Tanzania ambaye kwa sasa anachezea RB Leipzig ya Ujerumani kama winga na mshambuliaji.KWA NINI ANA ASILI YA TANZANIA?
Yussuf Yurary Poulsen anazaliwa na mama Mdenmark na baba Mtanzania. Baba yake Yussuf Yurary Poulsen (sasa matrehemu) alikuwa ni Muislam na ndiyo siri ya jina la Yussuf.
Baba yake alikuwa bahari wa Melini kwa safari za Tanga na Denmark kabla ya kuamua kuhamia mjini Copenhagen ambako ndiko umauri ulimkuta
Alifariki kwa ugonjwa wa saratani wakati Yussuf akiwa ana umri wa miaka minne tu. Yussuf amekuwa akizuru Tanzania mara kadhaa tangu mwaka 1996 akiwa mdogo na baadaye mwaka 2002, 2008 na 2011 mara ya mwisho.
Yussuf hakuwa hata mara moja kuitwa timu ya taifa ya Tanzania na ndiyo maana akachagua kuchezea Denmark nchi ya mama yake.

Yussuf Poulsen (katikati) akiwa na bibi yake mzaa baba (kulia) alipotembea na mpenzi wake (kushoto) mjini Tanga mwaka 2011 na chini akiwa na ndugu na jamaa upande wa marehemu baba yake. PICHA KWA HISANI YA MILARD AYO   

NAMNA ALIVYOIBUKA KISOKA
Kisoka aliibukia BK Skjold na mwanzoni Yussuf Yurary Poulsen alikuwa anacheza nafasi za ulinzi akiwa na mchezaji mwenzake rafiki yake, Kenneth Zohore ambaye baadaye walicheza naye pamoja timu za taifa za vijana za Denmark.

Baada ya Zohore kujiunga na FC Copenhagen, Yussuf Yurary Poulsen akahamia nafasi ya ushambuliaji BK Skjold kabla ya kujiunga na timu ya vijana ya Lyngby BK alipofikisha umri wa miaka 14.

Huko alicheza mechi yake ya kwanza timu ya wakubwa Desemba 4, mwaka 2011 alipoingia uwanjani dakika ya 84 akitokea benchi kuchukua nafasi ya Mathias Tauber katika mchezo na AC Horsens.
Haikuwa kazi rahisi kwa Yussuf Yurary Poulsen kupata namba katika kikosi cha kwanza, kwani hadi mwishoni mwa msimu aliishia kucheza mechi tano tu na klabu yake, Lyngby pia ikashuka kutoka Ligi Kuu ya Denmark.

Agosti 5, mwaka 2012 akafunga bao lake la kwanza katika timu ya wakubwa na klabu yake akicheza Ligi Daraja la Kwanza katika ushindi wa 1-0 dhidi ya AB Gladsaxe na tangu hapo akawa mchezaji wa kudumu kwenye kikosi cha kwanza akicheza jumla ya mechi 32 na kufunga mabao saba.

Yussuf Poulsen alijiunga na RB Leipzig Julai 3 mwaka 2013 ikiwa Daraja la Tatu Ujerumani

KUINGIA BUNDESLIGA
Mafanikio yake yakazivutia klabu nyingi za ndani na nje ya Denmark na haikuwa ajabu Julai 3 mwaka 2013 aliposaini mkataba na timu iliyopanda Daraja la Tatu Ujerumani, RB Leipzig.

Yussuf Yurary Poulsen akafanikiwa kuipandisha hadi Daraja la Pili Leipzig, baadaye la Kwanza kabla ya kuipeleka. Bundesliga mwaka 2016.

Na katika mechi yake ya sita tu ya Bundesliga msimu wa 2016–2017, akafunga bao lake la kwanza kwenye ligi hiyo kubwa zaidi Ujerumani katika ushindi wa 2–1 nyumbani dhidi ya FC Augsburg.


Yussuf Poulsen baada ya kuifungia bao pekee Denmark jana katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Peru

TIMU YA TAIFA YA DENMARK
Yussuf Yurary Poulsen alianza kuichezea timu ya taifa wa Denmark Oktoba 11, mwaka 2014 katika mchezo dhidi ya Albania kabla ya Juni 13, mwaka 2015 kufunga bao lake la kwanza kwenye mechi dhidi ya Serbia, Denmark ikishinda 2–0.
Yussuf Yurary Poulsen akateuliwa kwenye kikosi cha Denmark kilichocheza Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Joto mwaka 2016, ingawa alikataa uteuzi huo ili kupigania nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Leipzig.

Mei mwaka huu, akateuliwa kwenye kikosi cha Denmark cha wachezaji 23 wa mwisho kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi, kabla ya jana Juni 16 mwaka 2018 kuifungia bao pekee timu yake ya taifa katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Peru.

Huyo ndiye Yussuf Yurary Poulsen, mtoto wa baharia wa Tanga aliyenyimwa nafasi timu za taifa za Tanzania, ambaye sasa anaing'arisha Denmark Kombe la Dunia.

No comments:

Post a Comment