Wizi tanzanite watokea saa nane usiku - Karafuu24 Blog

Breaking

Monday, 25 June 2018

Wizi tanzanite watokea saa nane usiku


WIZI wa madini ya tanzanite, ambayo thamani yake bado haijajulikana, umetokea kwenye migodi ya tanzanite, Mirerani, wilayani Simajiro, majira ya saa 8 za usiku, Juni 21, mwaka huu.

Wizi huo umetokea huku serikali ikiwa imekamilisha ujenzi wa ukuta kuzunguka eneo la migodi hiyo na kuweka kamera za kisasa kuwanasa wanaopitisha madini hayo kwa njia ya wizi.

Ukuta huo wenye urefu wa kilomita 24.5 ulijengwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuzunguka eneo la migodi ya tanzanite na ukazinduliwa na Rais John Magufuli, Aprili 6, mwaka huu.

Ulijengwa na kuwekwa kamera za kisasa kwa lengo kudhibiti wizi wa madini hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Augustino Senga, alithibitisha jana kutokea kwa wizi huo.

Alisema wizi huo ulifanywa Juni 21, mwaka huu, majira ya saa 8 usiku na wahusika wote walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Alisema suala likishafika mahakamani wao hawawezi kulizungumzia, lakini wanaendelea na upelelezi zaidi juu ya tukio hilo.

Habari zilizopatikana zilisema, kikundi cha baadhi ya wafanyabiashara wa madini hayo kinachodaiwa kuchimba kwa njia haramu, ndicho kilichofanikiwa kuiba na kupitisha tanzanite geti kuu bila kulipia ushuru wa serikali.

Hata hivyo, habari zimesema wachimbaji 11 na wafanyakazi kadhaa wa kampuni moja ya uchimbaji madini Tanzanite One wamekamatwa kufuatia kutoweka kwa madini hayo.

Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Kaskazini, Adam Juma, alisema ofisi yake ilipokea kiasi cha kilo moja.

Hata hivyo, kamishna huyo alikataa kutoa taarifa zaidi kuhusu wizi huo akisema uchunguzi wa namna wizi ulivyotokea bado unaendelea.

Kampuni ya Tanzanite One inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na wazawa kwa upande wake inachunguza kutokea kwa wizi huo.

No comments:

Post a Comment