WATUMISHI WA UMMA ZANZIBAR WATAKIWA KUFATA KANUNI NA MIONGOZO YA KIUTUMISHI ILI KULETA UFANISI KATIKA KAZI - Karafuu24 Blog

Breaking

Saturday, 23 June 2018

WATUMISHI WA UMMA ZANZIBAR WATAKIWA KUFATA KANUNI NA MIONGOZO YA KIUTUMISHI ILI KULETA UFANISI KATIKA KAZI


WATUMISHI wa umma nchini wamewatakiwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma ili kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kuleta ufanisi.
Mkurugenzi mwendeshaji na utumishi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo Amali  Zanzibar Omar Ali Omar alitoa wito huo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waajiriwa wapya walioajiriwa na wizara yake katika miaka ya 2017 na 2018 yaliyofanyika katika skuli ya Haile Selassie na kuhusisha watumishi wa mkoa wa mjini magharibi unguja.
Alisema iwapo watumishi hao watazingatia misingi ya ajira zao wataweza kutekeleza wajibu wao na kusimamia utendaji haki kikamilifu jambo litakaloleta tija katika utumishi wao.
Alisema kanuni za utumishi wa umma zinaelekeza kutolewa mafunzo kwa watumishi wapya wa taasisi na mashirika ya serikali hivyo watumishi hao wanapaswa kuwa makini na kutumia fursa hiyo kujifunza mambo mbali mbali yanayowahusu.
Alisisitiza kuwa iwapo watumishi wa umma watazingatia dhana za ukuu wa sheria, usawa wa sheria na matumizi mazuri ya madaraka wataweza kufanya kazi kwa weledi, ustadi na kuepukana na migogoro ya utumishi isiyo ya lazima.
“Sheria ya utumishi wa umma namba 2 ya mwaka 2011 pamoja na kuelezea haki alizonazo mtumishi, pia inasisitiza juu ya wajibu kwa waajiri wa hivyo wanapaswa kuzingatia na kuzisimamia wakati wote”, alieleza.
Awali akimkaribisha Mkurugenzi huyo, Mkurugenzi chuo cha utumishi wa umma Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Ali amesema mafunzo hayo ni sehemu ya hitaji la kisheria hivyo washiriki hao wanapaswa kuyazingatia ili waweze kuyatumia kikamilifu katika majukumu yao ya kila siku.
Amesema ili mtumishi yeyote athibitishwe na kuingizwa katika orodha ya watumishi wa umma ni lazima apatiwe mafunzo elekezi yatakayomjulisha mambo ya kufanya na yanayokatazwa katika utumishi wake na kuipongeza wizara ya elimu na mafunzo ya amali kwa kutekeleza hitaji hilo la kisheria.
“Swala la kuthibitishwa kazini ni la msingi na lazima kwa kila mtumishi kwani lina faida kubwa wakati mtumishi anapomaliza utumishi wake serikalini na ndio unaotumika katika kutengeneza mafao ya muajiriwa”, alisema Dk. Talib.
Wakiwasilisha mada katika mafunzo hayo wakufunzi kutoka chuo cha utumishi wa umma Zanzibar Abdallah Juma na Hassan Issa waliwataka watumishi hao kutofanya makosa wa kiutumishi katika maeneo yao ya kazi ili waepuke kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria ambazo baadhi yao zina madhara katika maisha yao ya kila siku.
Wameyataja baadhi ya makosa hayo kuwa ni pamoja na utoro kazini, wizi, uzembe, ubadhirifu wa mali za umma, kutowajibika na kuiletea sifa mbaya taasisi makosa ambayo yanaweza kuepukwa iwapo watumishi hao watazingatia kanuni na maadili ya utumishi.
Jumla ya watumishi 1195 wanatarajiwa kupatiwa mafunzo hayo miongoni mwa watumishi wapya walioajiriwa na wizara ya elimu na mafunzo ya amali Unguja na Pemba ambapo mafunzo kama hayo yameendeshwa katika mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja katika awamu mbili ndani ya mwezi huu.
Mwisho.
Mkurugenzi mwendeshaji na utumishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo Amali (WEMA) Omar Ali Omar (katikati) akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo ya waajiriwa wapya wa wizara hiyo (hawapo pichani) yaliyoendeshwa na chuo cha utumishi wa umma Zanzibar (IPA). Wa pili kulia ni afisa elimu mkoa wa mjini magharibi mwalim khatib muhsin tabia. (PICHA NA OFISI YA MKUU WA MKOA WA MJINI MAGHARIBI).

NA MWINYIMVUA NZUKWI

No comments:

Post a Comment