Serikali Yafunguka Kuhusu Mtanzania Anayeng'ara Kombe la Dunia Huko Urusi - Karafuu24 Blog

Breaking

Monday, 18 June 2018

Serikali Yafunguka Kuhusu Mtanzania Anayeng'ara Kombe la Dunia Huko UrusiDar es Salaam. Serikali imevunja ukimya kuhusu Mtanzania Yussuf Poulsen anayeng’ara katika Fainali za Kombe la Dunia, akitamba kwenye kikosi cha Denmark.

Mtanzania huyo mwenye uraia wa Denmark, ameweka historia katika fainali hizo nchini Russia, baada ya kufunga bao pekee dhidi ya Peru.

Kiwango bora cha Poulsen mwenye miaka 24, kimeiibua Serikali ambayo jana ilitoa tamko kuhusu wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza soka Ulaya.

Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Nchini Yusuph Singo, amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuweka utaratibu maalumu wa kutambua wachezaji wote wenye asili ya Tanzania wanaocheza nje ya nchi.

Singo alisema shirikisho hilo ndilo lenye dhamana ya kujua idadi ya wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza Ulaya ambao watawekewa utaratibu na Serikali ili kuitumikia timu ya Taifa.

“Serikali hatuwezi kujua kila mchezaji anayecheza Ulaya ndio maana kuna taasisi (TFF) ambayo pamoja na mambo mengine ya kiutendaji, inatakiwa kuweka mfumo mzuri wa kutambua wachezaji wetu wanaocheza nje ya nchi.

“Kwa mfano huyu Mtanzania anayecheza Denamrk hatukuwa tukimfahamu, kama vyama vyetu vya michezo vingekuwa na utaratibu mzuri wa kujua wachezaji gani wanacheza nje ingekuwa rahisi,” alisema Singo.

Mchezaji huyo juzi aliweka rekodi kwa kuifungia bao Denmark lililowafanya kuibuka na pointi tatu muhimu kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Peru katika hatua ya makundi.

Bao hilo ni la pili kwa nyota huyo kufunga mfululizo katika ngazi ya Taifa, siku chache zilizopita aliifungia Denmark bao moja kati ya mawili dhidi ya Mexico.

Poulsen alianza kikosi cha kwanza cha Denmark kilichokuwa kikiongozwa na Christian Eriksen wa Tottenham Hotspurs.

Mchezaji huyo katika jezi amekuwa akitumia jina la Poulsen, lakini amebadili na kuweka jina la baba yake, Yurary anayetoka mkoani Tanga. Awali, Poulsen alinukuliwa akidai ameshindwa kuitumikia Taifa Stars kwa kuwa hakuwahi kuitwa licha ya mara kwa mara kurejea nchini kuitembelea familia yake mkoani Tanga.

No comments:

Post a Comment