RC.AYOUB MOHAMMED AWAPONGEZA MASHEIKH NA VIONGOZI WENGINE WA DINI WA MKOA WA MJINI. - Karafuu24 Blog

Breaking

Monday, 11 June 2018

RC.AYOUB MOHAMMED AWAPONGEZA MASHEIKH NA VIONGOZI WENGINE WA DINI WA MKOA WA MJINI.


MJINI MAGHARIBI

VIONGOZI wa dini nchini wamepongezwa kwa juhudi wanazochukua kuimarisha amani ya nchi na imani za waumini wao ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani jambo linalochochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohammed Mahmoud ametoa pongezi hizo kwa wakati tofauti ofisini kwake Vuga alipokutana na masheikh, maimamu , wasimamizi wa misikiti na viongozi wa dini nyengine wa mkoa huo na kuwataka kuendelea na kazi hizo katika miezi mingine baada ya  kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Mheshimiwa Ayoub ameeleza kuwa ndani ya mwezi huo viongozi hao waliendesha shughuli mbali mbali zinazoimarisha dini, kuhamasisha umoja, ushirikiano na maelewano miongoni mwa jamii ya watu wa Zanzibar na nje ya nchi  jambo lililoendeleza utamaduni wa kuvumiliana kidini kati ya waumini wa dini ya kiislamu na dini nyengine ziliopo nchini.
Amesema katika kipindi hicho viongozi wa dini ya kiislamu na dini nyengine  walishirikiana kuwahimiza waumini wao kutunza amani ya nchi, kujiepusha na vitendo viovu vikiwemo vya udhalilishaji wa kijinsia jambo amabalo linapaswa kuendelezwa  na kuwaomba viongozi hao waendelee kuiombea amani ya nchi na viongozi wake ili waendelee kutimiza wajibu wao kwa jamii kikamilifu.
Amesema viongozi hao pamoja na wajibu wa kuhakikisha wanaimarisha imani za waumini wao, pia wana jukumu la kuhakikisha waumini wao wanakuwa mstari wa mbele kuimarisha amani, usalama na uvumilivu wa kidini miongoni mwa jamii ili kujiendeleza kimaisha.
Aidha amewapongeza waumini wa dini ya kiislamu kwa kushiriki katika ibada  ya funga na harakati nyengine za kidini kwa utulivu na unyenyekevu mkubwa jambo alilolitaja kuwa ni sehemu ya utamaduni wa watu wa Zanzibar ambalo linapaswa kuendelezwa kwa manufaa yao ya duniani kesho akhera.
Akizungumza katika kikao hicho Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga alimpongeza kiongozi huyo wa mkoa kwa kutambua mchango wa viongozi wa dini na kuahidi kuwa ofisi yake itaendelea kusimamia na kuratibu shughuli za dini ya kiislamu kwa uadilifu kwa lengo la kuondoa migongano ndani ya  jamii.
Sheikh Soraga ambae pia ni Katibu wa kamati ya amani kitaifa inayoundwa na viongozi wa dini mbali mbali Zanzibar amesisitiza kuwa juhudi zinazochukuliwa na viongozi wa serikali za kuhimiza amani na kuimarisha ulinzi na usalama wakati wote zinapaswa kuungwa mkono na viongozi hao kwa manufaa ya nchi na watu wake.

Nao masheikh hao mbali ya kupongeza utaratibu wa mkuu huyo wa mkoa wa kukutana na viongozi wa dini mara kwa mara, pia waliupongeza uongozi wa mkoa huo kwa juhudi inazochukua katika kuimarisha ustawi wa jiamii kupitia imani za wananchi wake.
Wamesema kwa kiasi kikubwa umoja na maelewano yaliyopo mkoani humo yamechangiwa na ufuatiliaji wa karibu wa viongozi wa mkoa katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi wake jambo walilosema wataendelea kuliunga mkono ili kupata jamii yenye imani na amani ambayo ndio chanzo cha maendeleo ya taifa.
Mkutano kati ya mkuu wa mkoa wa mjini magharibi uliofanyika katika ofisi za mkoa huo Vuga Zanzibar pia ulitumika kujadili namna bora ya kuendeleza jamii na kupunguza vitendo viovu ndani ya kipindi cha sikukuu kilihudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa kamati za usalama za mkoa huo pamoja na katibu tawala wa mkoa bi. Hamida Mussa Khamis.
Mzee George.

No comments:

Post a Comment