Polisi akamatwa kwa tuhuma za kumuua Muuguzi - Karafuu24 Blog

Breaking

Monday, 11 June 2018

Polisi akamatwa kwa tuhuma za kumuua Muuguzi


Muuguzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mwamazengo wilayani Misungwi amefariki dunia ikidaiwa ni kutokana na kipigo kutoka kwa askari wa Kituo cha Polisi Misungwi.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi  kwamba askari anayetuhumiwa anashikiliwa kwa mahojiano.

Kamanda Msangi alisema mwili wa Edock umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanza, Sekou-Toure kwa uchunguzi.

Taarifa kutoka kwa mashuhuda walisema wa tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Juni 9, zinaeleza kuwa Edock alikamatwa usiku na askari waliokuwa doria wakati akirejea nyumbani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, Masoud Hussein na Ramadhani Omar, wakazi wa kijiji cha Misungwi walisema wakiwa wanazunguka mitaani kupiga ngoma kuamsha watu kula daku usiku wa kuamkia Juni 9, walikutana na kundi la askari waliokuwa doria wakiwa na baadhi ya watu waliofungwa mikono kwa pingu.

“Tulisogea na kuwasihi askari wasiwapige, lakini wakatuamuru kuendelea na shughuli yetu,” alisema Hussein.

Naye Omar alisema kwa kuogopa ukali wa askari hao waliondoka eneo hilo na kwenda kumuamsha balozi wa nyumba kumi, Mwadawa Hamisi waliyemuomba kwenda kuwanusuru watu waliokuwa wanashikiliwa ambao baadhi walikuwa wakazi wa eneo hilo.

Alisema balozi huyo alikwenda na kwamba licha ya kumsihi askari kuacha kumpiga mtuhumiwa hakusikilizwa.

Alisema Edock alipopoteza fahamu na aliachwa eneo hilo, hivyo wao walitoa taarifa kituo cha polisi ili kupata msaada wa kumpeleka hospitali lakini hawakusaidiwa.

Akizungumzia tukio hilo, Mwadawa alisema: “Ilikuwa kama saa 7:10 usiku wa kuamkia Jumamosi nilipogongewa na wananchi wakiniomba kwenda kuwanusuru watu waliokuwa wakipigwa na polisi wa doria. Lakini juhudi za kumsihi askari huyo kuacha kumpiga mtuhumiwa ziligonga mwamba. Haya ni matumizi mabaya ya madaraka. Mamlaka husika inatakiwa kuchukua hatua.”

Aprili 3, polisi wa Kituo cha Igogo jijini Mwanza walidaiwa kusababisha kifo cha mtoto Halfan Lema (miezi sita), kwa kukosa huduma ya kitabibu baada ya kumshikilia mahabusu mama yake, Ashura Theonest (26) mkazi wa mtaa wa Ibanda kata ya Nyegezi jijini Mwanza kwa tuhuma za wizi wa simu.

No comments:

Post a Comment