NAWAKABIDHI SIMBA BARUA YENU KUTOKA KWA KOCHA KERR - Karafuu24 Blog

Breaking

Wednesday, 13 June 2018

NAWAKABIDHI SIMBA BARUA YENU KUTOKA KWA KOCHA KERR
Na Saleh Ally
KOCHA Dylan Kerr raia wa Uingereza aliondoka nchini akionekana ameshindwa kabisa kupata mafanikio na Simba waliona hakuwa na mwelekeo mzuri.
Kerr aliinoa Simba ikiwa na wachezaji wengi vijana ingawa kulikuwa na mchanganyiko wa wakongwe na bado mambo hayakwenda vizuri.

Viongozi wengi walifafanua suala la kuondolewa kwa Kerr kama kocha ambaye hakuwa makini, alitengeneza urafiki na wachezaji kupindukia hali iliyopunguza umakini na kusababisha kikosi chao kuyumba.

Viongozi wengi wa Simba walionyesha kwamba Kerr alikwama au alifeli, wakaamua kumtupia virago. Lakini misimu miwili iliyopita, ameonyesha ni kocha wa aina nyingine kabisa akiwa na Gor Mahia ya Kenya na sasa anatakiwa nchini Afrika Kusini.

Moja ya klabu iliyovutiwa na Kerr ni Mpumalanga Black Ace ambayo inaamini ataisaidia. Jiulize, kuondoka Simba Kerr amekuwa nyota, kwanini?

Maana ameiwezesha Gor Mahia mara mbili kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Kenya, imebeba Kombe la Shirikisho, pia imebeba misimu miwili Kombe la SportPesa Super Cup na kuweza kubeba kitita cha fedha na pia sasa wanatarajia Julai mwakani kwenda nchini England kuwavaa Everton ya England.

Huyu ndiye yule Kerr aliyekuwa Simba? Nini alikikosea alipokuwa Simba na kipi amekipatia akiwa na Gor Mahia?SALEHJEMBE imefanya mahojiano ya ana kwa ana na Kerr ambaye ameelekeza lawama zake nyingi kwa viongozi wa Simba huku akisisitiza suala la mabadiliko.

Kerr anasema anaweza kurejea siku moja Simba lakini sharti lake kubwa ni kuona viongozi kadhaa wa Simba wakiondolewa kwa kuwa anaona ni wakwamisha maendeleo.

Kerr anawaona viongozi hao akiwataja kwa majina ni tatizo kubwa na wataifanya Simba iendelee kubaki ilipo. Anaona viongozi hao wanafanya kazi kwa ajili yao na si klabu, ndiyo maana anasema kutakuwa na maendeleo Simba hadi wakiondoka.

Nimeona niufikishe ujumbe huu kama sehemu ya barua, maana maneno yake mengi niliyaona kama mtu anayeandika barua akitaka kufikisha ujumbe wake.

Kuingilia kazi ya kocha:
Kerr anaamini Simba ni timu kubwa na inahitaji kufanya mambo kitaalamu. Viongozi hawapaswi kuonekana wanajua zaidi ya kocha kwa kumtaka afanye wanavyotaka wao.
Anamtaja kiongozi mmoja ambaye sasa hafanyi kazi za Simba kwamba alikuwa tatizo kubwa kwa kuwa alipenda kufanya kila jambo na kuwa na uwezo wa mambo kuliko kocha.
“KIla mara anataka nifanye anavyotaka yeye, haiwezi kuwa sahihi. Hakuna maana ya kuwa na kocha wakati kuna kiongozi ana uwezo kikazi zaidi ya kocha, wabadilike,” anasema.

Kuchagua wachezaji:
Kerr anasisitiza, suala la kuchangia mchezaji gani acheze linabaki kuwa la kocha na si kiongozi.

“Kuna mchezaji usipomchezesha mechi mbili tatu, atakulaumu. Inawezekana aliwaaminisha viongozi wenzake ni mchezaji mzuri wakatoa fedha nyingi.
“Usipompanga wanakuona kama wewe ni tatizo, kumbe kweli hana uwezo. Ukishikilia msimamo wako, basi kuanzia hapo hamtaelewana na ugomvi unaanzia hapo,” anasema.

Ugomvi na wachezaji:
Kocha huyo mzaliwa wa mji wa Leeds nchini England anaamini wanadamu kupishana kwa mambo kadhaa au hata kauli ni jambo la kawaida.

Lakini anataka mambo yawe na mwisho, kama mlipishana basi mnaweza kuendelea na maisha kwa kurudisha uhusiano.

“Lakini viongozi wanagombana na wachezaji, baada ya hapo wananuniana. Niko Simba kuna kiongozi alikuja akitaka nisiwe namchezesha mchezaji fulani kwa kuwa alimuonyesha dharau. Nikamuambia ni suala la kiuongozi kama anaweza kuadhibiwa ni sawa. Lakini kabla, nitaendelea kumtumia kwa kuwa ana msaada na timu. Kuanzia hapo sikuelewana tena na kiongozi huyo. Kama bado wanafanya hivi, wabadilike.

Hawajui,wanajua:
Kerr anaweka msisitizo kwamba viongozi wa Simba si wataalamu wa mchezo wa soka ni viongozi na wanaweza kuwa na ushauri mzuri kutokana na uzoefu wao.
“Lakini hawawezi kujua zaidi ya kocha, wanaamini wanajua lakini hawajui. Wanalazimisha vitu visivyo sahihi na wakikataliwa wanadhani wamedharauliwa, jambo ambalo si sahihi.
“Hapa Kenya, nimefanikiwa kwa kuwa uongozi kuanzia kwa mwenyekitu wa klabu wamenipa nafasi ya kufanya kazi yangu, nikikosea basi wanaweza kuhoji lakini hawawezi kuhoji kabla sijakosea.


Kulazimisha usajili:
 Kocha huyo Mwingireza, analieleza suala la viongozi kuwa na wachezaji wao, linaweza kuwa jambo linalomchanganya sana kocha.

“Kiongozi anakulazimisha mchezaji fulani ni mzuri, anataka ajaribiwe. Ukifanya hivyo, utaona anakulazimisha kwamba ni mzuri na wanamhitaji. Mimi naona huyu mchezaji si sahihi, lakini hawanisikilizi na unakuwa unajiuliza, nani hasa ni kocha.

“Haya mambo yanaweza kuwa yanakwenda chinichini na watu hawajui. Lakini si viongozi wote wanaofanya hivi lakini ukweli ni lazima wabadilike ili kuifanya Simba kuwa na maendeleo.
“Kama kiongozi anaongoza Simba, basi ajue anatafuta maendeleo ya Simba na si maendeleo yake yeye binafsi na familia yake,” anasema.

Kerr amesisitiza, kama kocha aliondoka akiwa na uhusiano mzuri na wachezaji na wanachama ambao anaamini Simba ina kati ya wanachama na mashabiki bora kwa kuwa ni watu wenye subira.

“Wanachama na mashabiki wa Simba ni tofauti sana, wasikivu na wavumilivu. Hii ni nadra sana kuwapata watu wa namna hii duniani katika mchezo wa soka. Ndiyo maana nasisitiza, watendewe haki kwa viongozi kufanya kazi yao vizuri na kubadilika mara moja na kama haiwezekani, basi wengi waondolewe ili Simba ikimbie kwa mwendo sahihi kwenda kwenye maendeleo zaidi.”

No comments:

Post a Comment