Msichana anyongwa mchana kweupe, 9 mbaroni - Karafuu24 Blog

Breaking

Monday, 18 June 2018

Msichana anyongwa mchana kweupe, 9 mbaroni

MANUGWA Nkwabi (20), msichana na mkazi wa Kijiji cha Lubili wilayani Misungwi mkoa wa Mwanza ameuawa kikatili kwa kunyongwa shingo kwa kanga na watu wasiojulikana kwa kinachodaiwa kuwa ni imani za kishirikina.

Akielezea tukio hilo la kusikitisha mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema lilitokea Juni 13 mwaka huu, saa saba mchana katika kijiji cha Lubili wilayani Misungwi. Alisema inadaiwa Nkwabi alikuwa na msichana mwenzake wakitoka mlimani porini kukusanya kuni kwa matumizi ya nyumbani.

Kamanda Msangi alisema, wakati wakirudi nyumbani, njiani walikutana na kijana wasiyemfahamu aliyemshika Nkwabi aliyekuwa nyuma ya mwenzake na kumnyonga shingo kwa kanga akafa baada ya muda mfupi. “Baada ya mwenzake kushuhudia tukio na hali ile, alitupa kuni na kukimbia kwenda katika makazi ya watu kuomba msaada zaidi ambapo wananchi walikimbia kutoa msaada lakini walipofika eneo la tukio walikuta ameshakufa”, alisema.

Kamanda alisema uchunguzi wa awali wa tukio hilo umebaini mauaji ya msichana huyo yanatokana na imani za kishirikina na watu tisa akiwemo mganga wa kienyeji wamekamatwa. “ Upelelezi na msako mkali unaendelea kuhusiana na tukio hilo. Nawaomba wananchi wa maeneo hayo watulie wakati huu ambao tunaendelea na uchunguzi”, alisema Kamanda. Kamanda Msangi alisema mwili wa marehemu umeshafanyiwa uchunguzi na umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya maziko kijijini

No comments:

Post a Comment