Mlinzi auawa kwa kupigwa risasi na Majambazi baada ya kuvamia maduka - Karafuu24 Blog

Breaking

Friday, 22 June 2018

Mlinzi auawa kwa kupigwa risasi na Majambazi baada ya kuvamia maduka


Mkazi wa Kata ya Bugogwa wilayani Ilemela, aliyetambulika kwa jina moja la Saytaa ameuawa kwa kupigwa risasi kifuani wakati akijaribu kupambana na majambazi waliovamia maduka.

Akizungumzia tukio hilo, leo Juni 22, Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Ilemela, Khadija Nyembo amesema tukio hilo limetokea jana Juni 21 saa sita na nusu usiku.

Amesema baada ya mlinzi huyo kusikia mlio wa bunduki alienda sehemu ya tukio kutoa msaada wa kuwadhibiti wahalifu hao ndipo alipouawa.

Majambazi hao wanaodhaniwa walikuwa na silaha za moto walivamia duka la jumla la vifaa vya ujenzi na duka la nguo lililokuwa pia lina huduma za kifedha na kupora fedha kisha kumuua mlinzi huyo.

Nyembo ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa wilaya hiyo amesema: “Watu waliposikia mlio wa bunduki hawakutoka lakini yeye alienda, katika kupambana nao bila kuchukua tahadhari wakampiga risasi.”

Mwenyekiti wa Mtaa wa Bugogwa, Alphonce Bundege amesema, licha ya mtaa wao kuwa na askari wa doria lakini siku ya tukio walichelewa.

No comments:

Post a Comment