Mahakama Yaweka Zuio kwa Benki Zote Nchini Kutoa Pesa za Ruzuku CUF - Karafuu24 Blog

Breaking

Tuesday, 12 June 2018

Mahakama Yaweka Zuio kwa Benki Zote Nchini Kutoa Pesa za Ruzuku CUF

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeweka zuio la muda kwa benki zote nchini kutotoa pesa zozote za ruzuku ya Serikali kwa Chama cha Wananchi (CUF), hadi kesi zinazohusu mgogoro wa uongozi unaofukuta ndani ya chama hicho zitakapoamuriwa

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Wilfred Dyansobera, Ijumaa iliyopita kufuatia maombi yaliyowasilishwa na Bodi ya Wadhamini wa chama hicho, kambi ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

Bodi hiyo kupitia kwa mawakili wake Juma Nassoro na Daimu Halfani waliwasilisha mahakamani hapo maombi hayo, baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuruhusu ruzuku ya zaidi ya Sh.600 milioni.

Msajili wa Vyama alitoa kiasi hicho cha ruzuku kwa chama hicho, kambi ya Mwenyekiti wake wa Taifa anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, licha ya kuwepo kwa amri ya kumzuia kutoa ruzuku kwa chama hicho kambi yoyote.

Kufuatia maombi hayo, Jaji Dyansobera katika uamuzi wake wa Ijumaa ametoa amri ya kuzizuia benki zote nchini kutoa ruzuku ya Serikali kwa chama hicho kambi yoyote kulingana na uamuzi wake wa awali dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Kwa uamuzi huu chama hicho hakitaweza kutoa pesa yoyote katika akaunti zake zinazohusiana na ruzuku ya Serikali, hadi kesi zilizoko mahakamani zinazotokana na mgogoro huo wa uongozi zitakapoamuriwa.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment