KAMATI YA MWENGE YA MIKOA YA UNGUJA YAWATAKA WATU BINAFSI NA WADUA KUCHANGIA ILI KUFANIKISHA MBIO ZA MWENGE. - Karafuu24 Blog

Breaking

Thursday, 21 June 2018

KAMATI YA MWENGE YA MIKOA YA UNGUJA YAWATAKA WATU BINAFSI NA WADUA KUCHANGIA ILI KUFANIKISHA MBIO ZA MWENGE.

Wajumbe wa Kamati za mwenge za mikoa mitatu ya Unguja wamewataka watu binafsi, mashirika ya umma na binafsi kuendelea kutoa michango yao ili kufanikisha mbio za mwenge wa uhuru zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Wakizungumza katika kikao cha matayarisho ya mapokezi na ukimbizwaji wa mwenge huo katika Mikoa yao kilichofanyika katika ofisi za Mkoa wa Mjini Magharibi, wamesema kumekuwa na mwitikio mdogo wa baadhi ya taasisi zilizofikiwa jambo ambalo linaweza kutofikiwa kwa malengo.

Katibu Tawala Mkoa wa Mjini Magharibi Hamida Mussa Khamis amewaeleza wajumbe hao kuwa licha ya ofisi yake kufanya maombi ya mafuta ya mwenge kwa wadau mbali mbali bado kumekuwa na mwitiko mdogo kuliko ilivyo kuwa kwa miaka iliyopita na kuwaomba wajumbe wengine kutumia nafasi zao kushawishi wawekezaji waliomo katika maeneo yao ya utawala.
Amesema mbali ya mafuta katika mbio hizo mkoa au wilaya inatakiwa kuwa na akiba ya fedha ili kugharamia huduma mbali mbali zikiwemo za kuchangia miradi ya maendeleo inayopitiwa na mwenge huo kwa ajili ya ukaguzi, kuwekewa mawe ya msingi au kuzinduliwa.

Nae Mwenyekiti wa kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Vuai Mwinyi amewahimiza waratibu wa mwenge na watendaji wengine kuwa wabunifu katika utafutaji wa michango ili kupunguza mzigo mkubwa wa gharama za ukimbizwaji wa mwenge huo.
Aliwashauri viongozi wa idara na taasisi za Serikali kufikiria kurejesha michango ya hiyari kwa watendaji wa ofisi zao kila mwezi ili kujiandaa na mbio hizo zinazofanyika kila mwaka kwa Mikoa na Wilaya zote za Tanzania bara na visiwani.

Aidha ameeleza kuwa licha ya kuwepo kwa michango hafifu bado mikoa hiyo imejipanga kikamilifu kuukimbiza mwenge huo katika mikoa yao ambapo miradi mbali mbali ya maendeleo inatarajiwa kupitiwa na mwenge huo unaotarajiwa kuanza mbio zake katika mkoa wa Kusini Unguja kuanzia Juni 26 mwaka huu.

NA FATUMA MOHAMMED

No comments:

Post a Comment