GOR MAHIA WAZIMA NDOTO ZA SIMBA KUCHEZA NA EVERTON, WATWAA UBINGWA SUPER CUP - Karafuu24 Blog

Breaking

Sunday, 10 June 2018

GOR MAHIA WAZIMA NDOTO ZA SIMBA KUCHEZA NA EVERTON, WATWAA UBINGWA SUPER CUP


Na George Mganga

Mechi ya fainali ya SportPesa Super Cup imemalizika kwa mabingwa wa Ligi Kuu nchini Kenya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Afraha mjini Nakuru, Gor Mahia walitawala zaidi mchezo wakiwa na kikosi chao kamili huku Simba wakipata wakati mgumu kutengeneza nafasi za kufunga.

Gor Mahia wamejipatia mabao yao kupitia kwa Mshambuliaji wao hatari, Medy Kagere aliyefunga la kwanza katika dakika ya 6 tu ya mchezo na kufanya kipindi cha kwanza kiende kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza tena kwa Gor Mahia kuzidi kulisakama lango la Simba wakionesha njaa ya kupata goli jingine ambapo mnamo dakika ya 54, Tuyisenga alifunga bao la pili kwa kumalizia mpira wa krosi uliopigwa kutoka kulia mwa Uwanja na kumuacha Kipa Aishi Manula akiwa hana cha kufanya.

Mpaka Mwamuzi wa mchezo anapuliza kipyenga cha kumaliza mchezo, Gor Mahia 2, Simba SC 0.

Ushindi huo unawafanya Gor Mahia kuwa mabingwa wa Kombe la SportPesa Super Cup kwa mara ya pili mfululizo na kujipatia tiketi ya safari kuelekea England kukipiga na Everton kwenye Uwanja wa Goodison Park.

Ikumbukwe mwaka jana Gor Mahia waliweza kutwaa ubingwa huo katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam baada ya kuwafunga wapinzani wao wa Kenya, AFC Leopards kwa jumla ya mabao 3-0.

No comments:

Post a Comment