DR.SHEIN AMTUMI SALAMU ZA PONGEZI RAISI WA DJIBOUT KWA KUTIMIZA MIAKA 41 YA UHURU WA TAIFA HILO. - Karafuu24 Blog

Breaking

Wednesday, 27 June 2018

DR.SHEIN AMTUMI SALAMU ZA PONGEZI RAISI WA DJIBOUT KWA KUTIMIZA MIAKA 41 YA UHURU WA TAIFA HILO.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Djibout, Ismail Omar Guelleh kwa kutimiza miaka 41 tokea Taifa hilo kupata uhuru wake.

Salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu zao wa Djibout katika kusherehekea siku hii adhimu  kwa Taifa hilo.

Kwa niaba yangu binafsi, watu wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar natumia fursa hii kukupongeza wewe pamoja na wananchi wote wa Djibouti kwa kutimiza miaka 41 ya uhuru, ilieleza sehemu ya salamu hizo alizotuma Dk. Shein.

Aidha, katika salamu hizo, Dk. Shein alimuhakikishia Rais Guelleh kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na Djibout sambamba na kuimarisha udugu uliopo kati ya wananchi wa pande mbili hizo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein katika salamu hizo alieleza kuwa miaka 41 ya uhuru wa Taifa hilo inaimarisha zaidi mashirikiano kati ya nchi mbili hizo pamoja na watu wake.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia nafasi hiyo kumtakia uongozi mwema Rais Ismail Omar Guelleh pamoja na kusherehekea vyema siku hii adhimu kwa Taifa hilo sambamba na kuendelea kuliongoza kwa amani na utulivu mkubwa kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa Djibout.

Djibout ilipata uhuru wake mnamo mwezi Juni mwaka 1977 kutoka koloni la Ufaransa chini ya kiongozi wake Hassan Gouled Aptidon ambaye alikuwa Rais wa kwanza wa Djibout.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment