DR.SHEIN AMTUMIA SALAMU ZA PONGEZI RAISI WA MSUMBIJI FELIPE NYUSI - Karafuu24 Blog

Breaking

Tuesday, 26 June 2018

DR.SHEIN AMTUMIA SALAMU ZA PONGEZI RAISI WA MSUMBIJI FELIPE NYUSI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Msumbuji, Felipe Nyusi kwa kutimiza miaka 43 tokea kupata Uhuru kwa Taifa hilo.

Salamu hizo zilieleza kuwa kwa niaba yake Dk. Shein, wananchi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wanaungana pamoja na ndugu zao wa Msumbuji katika kusherehekea siku hiyo adhimu ya uhuru wa Taifa hilo.

Aidha, katika salamu hizo, Dk. Shein alimuhakikishia Rais Nyusi kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na nchi hiyo sambamba na kuimarisha udugu uliopo kati ya wananchi wa pande mbili hizo.

Pia, salamu hizo zilieleza namna ya Zanzibar itakavyoimarisha ushirikiano uliopo kati yake na Msumbuji kwa kukuza uhusiano mwema wa kikanda na kimataifa.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumtakia Rais Nyusi afya njema yeye na familia yake na kumtakia maisha marefu yenye furaha pamoja na sherehe njema ya siku hiyo adhimu ya uhuru wa Taifa hilo kwa amani, utulivu na upendo kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa Msumbiji.

Msumbiji ilipata uhuru wake Juni 25 mwaka 1975 kutoka kwa koloni la Wareno chini ya Jamedari wake Samora Machel ambaye hatimae ndiye aliekuwa Rais wa kwanza wa Msumbuji huru.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment