Serikali kujenga makumbusho ya marais wastaafu - Karafuu24 Blog

Breaking

Thursday, 19 April 2018

Serikali kujenga makumbusho ya marais wastaafu


Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kujenga makumbusho ya Marais Wastaafu jijini Dodoma pamoja na kuanzisha makumbusho ya meno ya tembo katika miji ya Dar es salaam, Arusha na Dodoma zikiwa ni harakati za kukuza na kuimarisha sekta ya Utalii nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma.
Kingwangalla amemueleza balozi Cooke kuwa, Serikali kupitia Wizara yake inaendelea kuimarisha vivutio vya utalii hapa nchini kwa kupanua jeografia ya maeneo ya utalii sambamba na kuongeza vivutio ili kuongeza idadi ya watalii na mapato.
Sambamba na hayo amesema Serikali itaanzisha mwezi maalum wa maadhimisho ya urithi wa Mtanzania ambao utafanyika mwezi Septemba kila mwaka pamoja na kuendeleza utalii wa mikutano.
Amesema Serikali itaanzisha Mamlaka ya Usimamizi na Uendelezaji wa Fukwe nchini ili kuimarisha utalii wa fukwe pamoja na kutambua barabara iliyokuwa ikitumika katika biashara ya utumwa wakati wa ukoloni ili iweze kutumika kiutalii.

No comments:

Post a Comment