Makamanda Boko Haram wajisalimisha - Karafuu24 Blog

Breaking

Saturday, 21 April 2018

Makamanda Boko Haram wajisalimisha


Makamanda wawili wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameripotiwa kujisalimisha kwa jeshi la Serikali katika eneo la Maiduguri nchini Nigeria.
Taarifa ya kujisalimisha kwa makamanda hao imetolewa na Meja, Jenerali Rogers Nicholas alipokuwa akiwawasilisha rasmi wapiganaji hao wa Boko Haram kwa Serikali.
Jen. Nicholas ameongeza kuwa mbali na makamanda hao, wengine waliojisalimisha ni pamoja na kiongozi mwanamke na watoto watatu wanaotumiwa na kundi hilo katika eneo la Kumshe, Bama katika jimbo la Borno.
Alisema kuwa wapiganaji hao waliwasilisha barua yao ya kuomba kujisalimisha katika dawati maalum la Serikali, chini ya uangalizi maalum wenye usiri mkubwa wa kuhakikisha wanakuwa salama.
Jenerali huyo alisema kuwa jeshi lilianza kufanya mawasiliano na wapiganaji hao kwa njia maalum likiwatia moyo kujisalimisha na kwamba kuna kundi lingine kubwa la wapiganaji watakaojisalimisha baadaye.
“Kazi yetu ni kulinda maisha ya watu na mali zao, tunawataka wengine wajisalimishe kutoka msituni, waungane na jitihada za kuimarisha amani,” alisema Jenerali Nicholas.
Amesema baada ya kujisalimisha, Serikali imeandaa mpango maalum wa kuwapa mafunzo ya kuwaweka vizuri kisaikolojia kwa lengo la kuwaandaa kuchangamana na jamii kama watu wa kawaida kwa maendeleo ya taifa hilo.

No comments:

Post a Comment