MAKALA / MWANZO Ushirikina watumika kuuwa kesi Pemba - Karafuu24 Blog

Breaking

Thursday, 19 April 2018

MAKALA / MWANZO Ushirikina watumika kuuwa kesi Pemba


“WANAOLAWITI watoto sasa watumia mbinu nyengine ya ushirikina kuuwa kesi” hayo ni maneno ya mama mwenye miaka 45 makaazi wa Mchangamdogo Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
“Nilivimbishwa miguu ili nisiweze kuhudhuria mahakamani kufuatilia kesi ya mwanangu, ingawa nilijikokota kuhakikisha haki yangu naipata”, alisema kwa uchungu mama huyo.
Huku machozi yakimtiririka mama huyo, alisema licha ya kujitoa na maradhi aliyokuwa nayo kuifuatilia kesi yake, lakini jitihada zake hazikuzaa matunda, kwani mpaka wakati anafikiwa na makala hii kesi yake haijatolewa hukumu.
Ingawa juhudi za mama huyo za kufuatilia kesi ya mwanawe zimegonga ukuta kutokana na kuwa hadi sasa kesi hiyo imekwama kutolewa hukumu, jambo ambalo linamsababishia kutokwa na machozi kila anapofikiria.
Kinachomshangaza mama huyo, ni kuona kwamba inakaribia mwaka  tangu kumaliza kutolewa ushahidi kesi hiyo, ingawa mtuhumiwa hajatiwa hatiani, huku akitembea mitaani kwa mapana na madaha.
“Hivi tunaelekea wapi kama sio kuendeleza matendo ya ulawiti, tunawapa nguvu wanaotudhalilishia watoto wetu, kwani kesi tayari ishamaliza kusikilizwa mashahidi, lakini mpaka saivi nazungumza na wewe mwandishi hukumu haijatolewa”, alisema.
Mama huyo, anaeleza kuwa wakati alipokuwa anasimamia kesi ya mwanae, alikuwa akiumwa huku miguu ikivimba, hali ambayo ilimsababishia maumivu makali wakati anapotembea.
“Miguu ilikuwa inavimba mpaka kutembea siwezi na ni siku ile tu ninayohitajika kwenda mahakamani, nikirudi napoa na kuwa mzima kama chuma, hali hii ilinitisha sana ingawa sikukata tamaa”, alieleza mama huyo.
Alihakikisha kuwa, ushirikina unachangia kuuwa kesi hizo, kwani inakaribia mwaka bado hukumu haijatolewa, hali inayopelekea wanaofanya udhlilishaji kuendelea kuwafanyia ukatili huo watoto wadogo.
“Ushirikina ukiendelea kufanywa kwa ajili ya kuua kesi hizi, matendo hayo yatashamiri katika jamii, kwani wengine wakiumwa kama nilivyoumwa mimi basi wanasamehe kusimamia kesi zao”, alisema mama wa mtoto huyo.
Ushirikina ni jambo ambalo litapelekea watu wenye nia ya kwenda kutoa ushahidi, kushindwa kwa kuepuka kufanyiwa mambo ya kichawi na kuwaomba wanawake wenzake kuiga mfano wake, ili kuhakikisha ukatili kwa watoto unaondoka kwenye jamii.
Anaeleza kuwa, baada ya ushahidi kukamilika waliambiwa kinachofuata ni kutolewa hukumu kesi hiyo, ingawa inaenda na kurudi bila ya mtuhumiwa huyo kutiwa hatiani.
“Tushaitwa mahakamani zaidi ya mara mbili kwenda kwa ajili ya kutolewa hukumu ya kesi hiyo, lakini tukifika tu tunaambiwa njooni siku nyengine leo haitolewi hukumu”, alieleza kwa maskitiko mama huyo.
Mama huyo, alielezea sababu ya kufanyiwa ushirikina ni kutokana na kuwa hakukubali kufanya suluhu, wakati walipokwenda wazazi wa mtuhumiwa kumtaka wayamalize bila kupelekwa Mahakamani.
“Wilikuja wanafamilia ya mtuhumiwa, lakini sijakubali suluhu kwa kesi kama hii, kwani nilihofia kwa mtoto wangu kuniona adui wakati akaiwa mkubwa, kwani ataambiwa na watu ‘mama yako alichukua pesa,  ulipolawitiwa’ kwa kweli asingenithamini”, alisema.
Ni changamoto nyingi zinazomkumba mwanawe, tokea kufanyiwa kitendo cha ulawiti, ikiwa ni pamoja na watoto wenzake kumnyanyapaa kimaneno, jambo ambalo linasababisha kukosa furaha wakati wote, hasa akiwa skuli.
“Kwa kweli upatikanaji wa elimu kwa mwanangu utakuwa ni wa shida sana, maana wanapokuwa skuli watoto wenzake humchokoza na ndipo anapokuja kuniuliza mimi, ingawa humwambia sio kweli wala asiwasikilize”, alieleza huku machozi yakimuelea kwenye macho yake.
Mtoto huyo, alifanyiwa kitendo cha ulawiti akiwa na miaka mitatu, ambapo tukio hilo lilitokea mwaka 2015 hadi sasa kesi hiyo haijatolewa hukumu.
“Kuna siku alikuja na kuniuliza eti mama, mimi nilifanyiwa ulawiti nilipokuwa mdogo? lakini nikamwambia sio kweli, naviomba vyombo vya sheria vitende haki, ili mwanangu apungue kudhalilika”, alihadithia mama huyo.
Katika kumbu kumbu za mtoto huyo wakati anapochokozwa na watoto wenzake skuli, humwambia mama yake kuwa ‘mama nakumbuka nilipokuwa mdogo nilikwenda sehemu kuna askari na kupanda juu ya meza na kuulizwa maswali’ jambo ambalo linamtia huzuni mama yake kila akifikiria.
“Huku mwanangu ameshadhalilishwa na bado mtuhumiwa anatembea mitaani kwa mapana, hii inauma sana, kama mahakama haiwezi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria watuachie wanajamii tuhukumu wenyewe tunapowakamata, tumechoka”, alisema mama huyo.
Uchunguzi wa makala hii umebaini kuwa, kesi ya mtoto huyo katika kituo cha Polisi ilipewa namba CCR namba 151 ya mwaka 2015 na Mahakama ya watoto namba 4 ya mwaka huo.

Siti Khatib Ali ambae yeye ndie Mratibu wa wanawake na watoto anaeshughulikia shehia hiyo, alisema kesi hiyo ilikwenda mahakamani na mashahidi wote walisikilizwa, ingawa imekwama kutolewa hukumu hadi sasa.
“Kwa kweli sijui kesi hiyo inakwamishwa na nini, maana ishafika wakati wa kutolewa hukumu lakini kila siku inapangiwa tarehe nyengine, hiyo hukumu sijui itatolewa lini, hii inaumiza sana”, alisema.
Mratibu alisema suala la kuwepo ushirikina wa kukwamisha kesi hizo, unaweza kuwepo, kwani katika jamii kuna kila vituko ambavyo hufanyiana.
“Mama huyu alikuwa anaumwa na miguu wakati akienda kwenye kesi, lakini yeye mwenyewe ndie anaejua kwamba ni ushirikina au la, mimi naiomba serikali isicheleweshe kesi hizo kwa kusikilizwa na kutolewa hukumu”, alisema mratibu.
Alifafanua mratibu, shehia hiyo kipindi cha mwaka 2015 hadi mwaka huu imeripotiwa kesi moja ya ulawiti, ingawa kuna watoto 12 walituhumiwa kulawitiana wao kwa wao, mara baada ya kutajana baada ya mmoja wao kugunduliwa na kaka yake akijichezea sehemu zake za siri.
“Watoto hao ni kati ya miaka minne mpaka saba, hivyo jamii ielewe wanapofumbia macho kesi hizi pamoja na mahakama kuchelewesha kutoa hukumu, basi watoto wetu wako katika hatari kubwa ya kulawitiwa”, alisema kwa uchungu mratibu.
“Kwa sababu tuangalie kwa undani, hivi zaidi hawa watoto 12 wamefundishwa na nani mchezo huo, ukija kugundua kumbe yupo mtu mzima, hivyo tunaiomba serikali iwachukulie hatua za kisheria wale wote wanaobeza kesi hizi”, alizidi kufafanua.
Mratibu anaeleza, shehia yake ni miongoni mwa shehia sita zilizopata elimu ya kupinga matendo ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto kupitia mradi wa kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake GEWE.
“Mradi huo upo chini ya chama cha waandishi wa habari wanawake TAMWA, ambapo wamekuwa wakichukua juhudi kubwa ya kutoa elimu kwa wanajamii, juu ya kupiga vita udhalilishaji, ingawa jambo linalorudisha nyuma ni kutokana na kucheleweshwa kutolewa hukumu kwa kesi hizo”, alisema.
Ni mradi ulioingia kwenye shehia sita za Wilaya ya Wete pekee kwa kisiwa cha Pemba, ambazo ni Kinyikani, Mchangamdogo, Kiungoni, Shengejuu, Kangagani na Mjini Ole, ambao umekuwa ukiwaelimisha wanajamii juu ya kuviripoti na kuvikemea vitendo hivyo, ili visiendelee kuwepo.
Haroub Suleiman Hemed ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Wete, alisema kuwa jambo kubwa linalowakwaza ambalo linapelekea kuongezeka kwa kesi hizo ni kuchelewa kutolewa hukumu.
“Ucheleweshwaji wa kesi kutolewa hukumu unaiathiri sana jamii na Taifa kwa ujumla, wanajamii hufikia mpaka kukata tamaa kufuatilia kesi, sasa ni wakati muafaka kwa mahakama kubadilika, wanajamii wamechoka”, alisema kwa uchungu.
Haroub alieleza, kesi nyingi hukwama zinapofika mahakamani, ambapo hawajui kitu kinachokwamisha kesi hizo na kupelekea watuhumiwa kutembea kwa mapana mitaani huku wakiendelea kulawiti watoto.
“Mradi wa GEWE umetoa elimu kwa shehia ya Mchangamdogo, Kinyikani, Shengejuu, Kiungoni, Kangagani na Mjini Ole kwa wajamii juu ya kuripoti vitendo hivyo, ingawa kinachorudisha nyuma juhudi zao ni kutokana na kucheleweshwa kutolewa hukumu kwa kesi hizo”, alisema Afisa Haruob.
Ofisi ya Ustawi wa Jamii Wilaya ya Wete ilipokea kesi 15 za ulawiti waliofanyiwa watoto, kuanzia mwaka 2015 hadi Novemba mwaka huu.
Mwanasheria dhamana kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Pemba, Ali Rajab Ali alifafanua kuwa, kwa sasa sheria imeweka wazi kwamba, yeyote anayejaribu kumlawiti mtoto wa kiume na Mahakama ikithibitisha, atakabiliwa na kifungo cha miaka 25 au akilawiti basi ni kifungo cha maisha jela.

Ingawa anaeleza, pamoja na vurumai ya ulawiti iliopo, hadi sasa hakuna kesi ya ulawiti, mshitakiwa aliefungwa maisha, kwa sababu kesi hizo nyingi hufikishwa Mahakama za Mkoa, ambazo hazina meno kisheria.

Alieleza, kuanzia kipindi cha mwaka 2015 hadi mwaka huu, ofisi hiyo yenye mamlaka ya kushitaki kesi jinai, ilipokea kesi za ulawiti tisa (9), ambazo zinaendelea kusikilizwa mahakamani.

Wilaya ya Wete pekee ilipokea kesi 63 za watoto walifanyiwa kitendo cha ulawiti, ambapo Ustawi wa jamii kesi 15, Dawati la wanawake na watoto tisa, Ofisi ya DPP kesi tisa, Kituo cha mkono kwa mkono 13 mahakama ya mkoa Wete kesi 11 na shehia sita zilizofikwa na mradi wa GEWE zimeripotiwa kesi sita.

TAMWA katika harakati zake za kupinga vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto chini ya mradi wa GEWE, tayari imewapa elimu wanajamii wa Wilaya ya Wete kwa Pemba na Wilaya ya Magharibi na Kusini kwa Unguja, ili kuondosha kabisa vitendo hivyo, ambapo kwa sasa wanatanua wigo, ili kuhakikisha vitendo hivyo haviendelei katika jamii.
MWISHO.
Na Zuhra Juma , Pemba

No comments:

Post a Comment