KAMISEHNI YA UTALII NA IDARA YA MAKUMBUSHO ZANZIBAR ZATAKIWA KUTUMIA VYOMBO VYA HABARI KUITANAGAZA HISTORIA YA NCHI - Karafuu24 Blog

Breaking

Friday, 20 April 2018

KAMISEHNI YA UTALII NA IDARA YA MAKUMBUSHO ZANZIBAR ZATAKIWA KUTUMIA VYOMBO VYA HABARI KUITANAGAZA HISTORIA YA NCHI

Related image
KAMISHENI ya Utalii Zanzibar na Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale, zimetakiwa kuvitumia kikamilifu vyombo vya habari katika kuitangaza historia ya nchi na vivutio vya utalii vilivyomo Unguja na Pemba.
Akizungumza na uongozi na wafanyakazi wa Kamisheni ya Utalii huko Amani katika muendelezo wa ziara zake kuzitembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Waziri  Mahmoud Thabit Kombo, amesema sio vyema sekta hizo tatu kufanya kazi kila moja pekee.
Alieleza kuwa, hatua ya kuunda wizara inayoziweka pamoja sekta hizo, ilenge kuziunganisha na kufanya kazi kwa pamoja ili kuutangaza utalii wa Zanzibar, vivutio, magofu na mambo mengine ya kale ambayo yana thamani kubwa inayoweza kuitajirisha nchi iwapo yatauzwa kupitia vyombo vya habari.
Waziri Kombo alisema, mbali na vyombo vya habari vya serikali ambavyo viko chini ya wizara moja na Kamisheni ya Utalii na Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale, vyombo binafsi pia vinapaswa kuhamasishwa kuutangaza utalii wa Zanzibar.
“Udhaifu unaoonekana, ni kwamba hakuna muunganiko wa vyombo vya habari, Kamisheni ya Utalii, Idara ya Mambo ya Kale na Makumbusho, na hili ndilo linaloyumbisha utalii wetu licha ya juhudi za kuinua maeneo mengine yanayohusiana na sekta hiyo,” alifafanua Waziri Kombo.
Alieleza kuwa, umefika wakati watendaji wakuu wa sehemu hizo kwa kushirikiana na uongozi wa wizara, kukaa pamoja na kuandaa mkakati madhubuti ili kuhakikisha maeneo hayo yanaimarishwa, huku vyombo vya habari vikitoa muda wa kutosha kuzitangaza programu za utalii nchini.
Waziri Kombo alisema Zanzibar imejaaliwa utajiri mkubwa wa rasilimali na historia za kale ambazo ni lulu kwa watalii na wageni wengiue wanaiofika ncini, lakini ni lazima zitangazwe vizuri na kuengwaengwa, ili kupandisha hadhi ya utalii wa visiwa hivi, hali itakayoongeza mapato ya serikali na ustawi wa wananchi. 
“Ninafahamu kuna changamoto nyingi zinazokwamisha malengo yetu, lakini ninaamini tukifanya kazi kwa kutumia maarifa na rasilimali tulizonazo, mipango yetu ya kuongeza idadi ya watalii na nchi zinazowaleta itafanikiwa,” alisema.
Hata hivyo, aliieleza Kamisheni hiyo, kuwa pamoja na changamoto mbalimbali inazokabiliana nazo, serikali inaridhika na juhudi inazofanya kutanua wigo wa utalii wa Zanzibar, hasa kwa kuongeza idadi ya watalii na masoko mapya kutoka nchi nyengine, sambamba na kuongezeka kwa muda wa watalii hao kukaa nchini.
Waziri Kombo aliiagiza Kamisheni hiyo kuhakikisha hadi ufikapo mwisho wa mwaka  huu 2018, Zanzibar iwe na mawakala wa utalii katika nchi za Uturuki, Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), Italia, Misri, Oman, Ukraine na Israel ambazo zimeonesha nia ya kushirikiana na Zanzibar, mbali na ule ulioko nchini India.
Mapema, akisoma taarifa ya Kamisheni, Mkurugenzi Mipango na Sera Ashura Mrisho Haji, alitaja changamoto mbalimbali zinazozorotesha utendaji wao, ambazo ni uhaba wa usafiri, ugumu wa wadau wa utalii katika kutii sheria na mgongano wa sheria baina ya taasisi za serikali katika kukusanya mapato yatokanayo na biashara ya utalii.
Nyengine ni maslahi madogo ya wafanyakazi kulinganisha na majukumu ya taasisi pamoja na mchango mkubwa wa sekta ya utalii kwa uchumi wa taifa, na upatikanaji wa takwimu sahihi za watalii wanaoingia nchini.
Lakini alisema, kuundwa kwa kamati ya ushauri juu ya masuala ya utalii inayohusisha ngazi tafauti ikiwemo ya shehia, kumesaidia pakubwa kubaini baadhi ya matatizo yanayoikwaza sekta hiyo na kuyatafutia ufumbuzi unaofaa.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Kamisheni hiyo Dk. Vuai Iddi Lila pamoja na Ofisa Masoko Dk. Miraji Ukuti Ussi, waliahidi kuyafanyia kazi maelekezo ya Waziri Kombo ili kuhakikisha sekta ya utalii inapata mafanikio zaidi kwa manufaa ya nchi na wananchi wake.
Waziri Kombo pia alilitembelea Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, ambako alisisitiza umuhimu wa kulipwa madeni inayodai kwa wateja wake zikiwemo taasisi za serikali, ili nalo liweze kuwalipa wachapishaji wake kwa wakati.
Na Salum Vuai, MAELEZO

No comments:

Post a Comment