Israel yaadhimisha miaka 70, yawaonya maadui zake - Karafuu24 Blog

Breaking

Thursday, 19 April 2018

Israel yaadhimisha miaka 70, yawaonya maadui zake


Israel imeanza maadhimisho ya kutimiza miaka 70 tangu kuundwa kwake ambapo waziri mkuu wa nchi hiyo, Benjamin Netanyahu ametumia maadhimisho hayo kuwaonya maadui zake na kugusia mahusiano na baadhi ya mataifa ya Kiarabu.
Netanyahu amezindua maadhimisho ya uhuru wa Israel usiku wa jana Jumatano katika sherehe za kuwasha mwenge, na kutoa vitisho kwa Iran pamoja na kutoa mkono wa mshikamano kwa wale wanaotaka amani.
Amesema kuwa Israel inakabiliwa na mgogoro wa uchochezi kutoka kwa jirani zake, ambao wengi wao wanakataa kukubali uwepo wa taifa hilo mashariki ya kati na kuonya kwamba yeyote atakayeinua mkono dhidi ya Israel hatosalimika.
Aidha, Netanyanhu ameusifia uamuzi wa rais wa Marekani, Donald Trump alioutoa mapema mwaka huu kuhusu Israel akisema kuwa, wote wanausifu uamuzi wa kihistoria wa Rais huyo wa kuitambua Jerusalem kama mji mkuu na kuuhamisha ubalozi wa taifa lenye nguvu duniani.
Hata hivyo, mvutano kati ya Israel na Iran unazidi kuongezeka juu ya uwepo wake nchini Syria na ishara kwamba uadui wa miongo kadhaa baina ya Israel na mataifa ya kiarabu ya Ghuba unazidi kushika kasi kitu ambacho kinazidi kuzua wasiwasi katika eneo la mashariki ya kati.

No comments:

Post a Comment