Dk. Shein: Sikuingilia uhuri wa ZEC - Karafuu24 Blog

Breaking

Wednesday, 18 April 2018

Dk. Shein: Sikuingilia uhuri wa ZEC


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na ujumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ulioongozwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, ambaye alikabidhi ripoti ya utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo, hafla hiyo ilifanyika jana Ikulu mjini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa kutekeleza vyema majukumu yake ndani ya miaka mitano.
Aliyasema hayo jana baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha akiwa amefuatana na wajumbe wa tume hiyo kumkabidhi ripoti ya utekelezaji kwa kipindi cha miaka mitano kilichoanzia Aprili 30, 2013 mpaka Aprili 29, 2018 ambapo wajumbe hao wanafikia ukomo.
Dk. Shein alisema ZEC inapaswa kupongeza kwa kusimamia na kuendesha vyema chaguzi huku Zanzibar ikiendelea kuwa yenye amani na utulivu.
Alisema tume hiyo imefanikisha vyema kazi waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuendesha chaguzi zote ukiwemo uchaguzi mkuu, chaguzi ndogo na ule uchaguzi wa marudio ambazo zote hizo zilifanywa kwa ufanisi mkubwa.
Alisema ZEC ilionesha juhudi na ilikuwa imara huku ikisimamia katiba, sheria na kanuni za tume hiyo na kusisitiza kuwa kwa niaba ya serikali na wananchi wote wa Zanzibar anaipongeza tume hiyo kwa mafanikio makubwa iliyoyapata.
Aidha, aliithibitishia tume hiyo kuwa ameipokea kwa furaha kubwa ripoti aliyokabidhiwa na tume hiyo na kueleza jinsi alivyoridhika na tume hiyo kutokana na utendaji wake wa kazi kwa kipindi chote cha miaka mitano.
Aliongeza kuwa katika kipindi chote cha miaka mitano ya tume hiyo hakuiingilia hata siku moja na aliiacha kufanya kazi zake  kwa uhuru na kuahidi kuwa hata tume ijayo hatoiingilia na itaendelea kuwa huru.
Alieleza kuwa taasisi hiyo iko huru na hakuna chombo chochote duniani kitakachoingilia katika kazi zake huku akiipongeza kwa jinsi inavyoendelea kupata heshima kubwa.
Alisema tume hiyo imeendelea kupata heshima kubwa duniani ikiwa ni pamoja na kuhudhuria katika vikao kadhaa vikiwemo vile vya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na vyenginevyo ambapo hiyo yote inatokana na jinsi inavyofanya kazi zake kwa viwango kikubwa.

No comments:

Post a Comment