BALOZI SEIF ALI IDDI AFANYA ZIARA MAALUMU YA KUKAGUA MAENEO YALIOATHIRIKA NA MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA - Karafuu24 Blog

Breaking

Saturday, 21 April 2018

BALOZI SEIF ALI IDDI AFANYA ZIARA MAALUMU YA KUKAGUA MAENEO YALIOATHIRIKA NA MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa tahadhari kwa Wananchi juu ya matumizi sahihi ya Pampas kwenye Mitaa ili kufuata Sheria na Kanuni za Afya zinazowajibikia kuzitekeleza katika mazingira yao ya kila siku bila ya kusubiri wakati wa miripuko ya maradhi ya kuambukiza.
Alisema endapo tahadhari hiyo haitachukuliwa ipasavyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaweza kuchukuwa hatua ya lazima ya kupiga marufuku uingizwaji wa bidhaa hiyo hapa Nchini kama ilivyofanya kwa Mifuko ya Plastiki ambayo imeleta afueni katika utunzaji wa Mazingira Nchini.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa  tahadhari hiyo wakati alipofanya ziara maalum ya kukagua maeneo yaliyoathirika na Mvua za Masika zinazoendelea kunyesha Nchini pamoja na kuona hali halisi ya Mazingira katika maeneo mbali mbali yaliyomo ndani ya Mkoa Mjini Magharibi.
Alisema Pampas ni vifaa vilivyotengenezwa Maalum kwa ajili ya uhifadhi wa uchafu wa Mwanaadamu, lakini baadhi ya Watu wameonyesha tabia mbovu ya matumizi ya vifaa hivyo kwa kuvitupa ovyo baada ya matumizi bila ya kuvipeleka katika maeneo maalum au kuvifukia.
Balozi Seif  alionya kwamba vitendo hivyo ambavyo vinaweza kuathiri Afya za Wananchi wengi vinafaa kudhibitiwa mara moja ili kuepuka  kutapakaa kwa miripuko ya Maradhi mbali mbali hasa Kipindu pindu kinachoibuka kutokana na vinyesi vinavyotupwa kiholela.
Balozi Seif akiridhika na Ujenzi wa Mtaro wa Maji machafu ya Mvua katika Shehia ya Karakana ambao umeleta ukombozi mkubwa wa kuondoka kwa mafuriko ya Mvua kwa Wananchi wa eneo hilo aliwashukuru Wananchi wa Kaya  Nne zilizojikubalisha kuvunjwa Nyumba  zao ili kupisha ujenzi wa Mtaro huo uliogharimu zaidi ya Shilingi Milioni Mia Moja.
Akikagua Daraja la Mwera Gudini lililokumbwa na kadhia ya mafuriko ya mvua za masika na kuleta athari kwa wapiti njia wa eneo hilo hasa Wanafunzi Balozi Seif  aliuagiza Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi na Wilaya zake kukaa pamoja na Wataalamu wa Ujenzi wa Madaraja ili kuangalia namna ya kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
Alisema  ni vyema kwa Wataalamu na viongozi hao wakashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi “B” kufanya utafiti wa ujenzi wa  Daraja hilo pamoja na kuangalia mazingira ya mteremko wa Maji yanayopita sehemu hizo  ili upatikane ufumbuzi wa pamoja na kuepuka kutapakaa kwa maji ya Mvua katika Makaazi ya Wananchi wa sehemu hizo.
Nao Wananchi wa maeneo hayo wameishuruku na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada inazochukuwa za kuwaondoshea kadhia Wananchi hao jambo ambalo wamepata faraja kubwa hasa katika yale maeneo yaliyokuwa yakifurika Maji.
Wananchi hao walisema zipo sehemu zilizopata ufumbuzi wa kuondoshwa kwa maji yanayotuwana kutokana na kujengwa miundombinu imara na hatimae kuwaondoshea hofu iliyokuwa ikiwatanda wakati wakiona dalili za wingu la mvua.
Hata hivyo wananchi hao waliiomba Serikali Kuu kuangalia pia athari zilizojichomoza katika maeneo mengine Nchini  hasa katika Miundombinu ya Bara bara ili faraja hiyo ienee kwa Wananchi waliowengi zaidi Unguja na Pemba.
Mapema Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed  Mahmoud alisema athari za Mwaka huu hazikuwa kubwa sana ikilinganishwa na Miaka iliyopita nyuma kutokana na uelewa wa Wananchi wa kujiepusha na athari zinazojitokeza wakati wa Msimu wa Mvua za Masika.
Mh. Ayoub alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hadi sasa Nyumba zilizoingia Maji zimekadiriwa kufikia Elfu 1,555, kati ya hizo Nyumba 447 ziliingia Maji na kutoka, Nyumba 1,900 zimehamwa na Nyuma 19 zimepata athari ya kukatika.
Alisema Uongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na vitengo vya Taasisi zote ulikagua Magenge 33,  ambapo 9 kati yake yako katika mazingira yanayokubalika Kiafya, Magenge 20 yamerekebishwa na kuendelea kutoa huduma na Magenge Manne yamezuiliwa kabisa kutoka na mazingira yake yasiyoridhisha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziba Balozi Seif na Ujumbe wake alikagua Daraja la Nyumba Mbili  liliopo Mwanakwerekwe  ambalo linamalizia utanuzi wake, alitembelea na kuona athari zilizojitokeza za athari ya Nyuma kutokana na kujaa kwa Maji katika Ziwa liliopo Fuoni Jangamizi.
Wananchi wa eneo hilo waliiomba Serikali Kuu kuangalia uwezekano wa kutafutiwa ufumbuzi tatizo hilo linaloendelea  na kuonekana kuongezeka kila Mwaka na kuleta kadhia .
Balozi Seif alimaliza ziara yake kwa kukagua eneo la Kibonde Mzungu ambalo Serikali hulazimika kufunga njia ili kuepuka maafa kutokana na kuongezeka kwa kina cha  Maji  kulingana na Mvua za Masika zinavyonyesha na hatiame kusababisha kuvuka kwa Maji upande wa pili wa bara bara.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifanya ziara kukagua maeneo mbali mbali yaliyoathirika na Mvua za Masika zinazendelea Nchini katika Mkoa wa Mjini Magharibi.
Wananchi wa Mtaa wa Mwera Gudini wakisubiri ujio wa  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyelenga kulikagua Daraja lao lililoleta athari kutoka na kasi ya Maji ya Mvua za Masika
Mkaazi wa Mwera Gudini Bwana Said Alex akimuelezea  Balozi Seif  kadhia inayowakumba wakati wanapovuka kwenye daraja lao ambalo bado linaendelea kuwa kero licha ya kujengwa kwa hatua za dharura.
 Balozi Seif  aliyevaa Kofia akiwapongeza Wananchi katika maeneo mbali mbali nchini kwa ustahamilivu wao waliochukuwa kutokana na kadhia ya mafuriko ya Mvua za Masika zinazoendelea kunyesha Nchini.
Balozi Seif na Viongozi wengine wa Serikali wakiangalia Mtaro wa maji machafu uliojengwa katika Mtaa wa Karakana ambao umeleta ukombozi kwa Wananchi wa eneo hilo.
Mzee Ame Nahoda Mkaazi wa Mtaa wa Karakana akielezea faraja yake na kuishukuru SMZ kwaniaba ya Wananchi wenzake kutokana na kujengewa Mtaro wa maji machafu ambayo yatakuwa Historia katika eneo lao.
Ziwa la Fuoni Jangamizini ambalo kujaa kwake maji  ya Mvua za Masika kunaendelea kuathiri Nyumba za Wananchi walio pembezoni mwa Ziwa hilo.
Picha na – OMPR – ZNZ
Othman  Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
21/4/2018.

No comments:

Post a Comment